Benki ya Dunia yatoa milioni 250 kupokonya silaha waasi
10 Januari 2023Fedha za ufadhili huo mpya zitakabidhiwa serikali ya Congo na kutekelezwa na taasisi ya kiserikali inayoitwa mpango wa kupokonya silaha PDDRC-S katika majimbo ya Ituri, Kivu kaskazini na Kivu kusini.
Ufadhili huo unalenga zaidi ya watu milioni 3 katika majimbo hayo matatu ya mashariki ya Congo, kwa nia ya kuzuia vijana kujiunga tena na makundi yenye silaha. Muda wa utekelezwaji bado haujatangazwa ila uongozi wa mpango wa kuwapokonya silaha wanamgambo na kuwarejesha katika maisha ya kawaida ya kijamii, kwa kifupi PDDRC-S, umesema kila kitu kilikuwa tayari, na kwamba pesa hizo zilikuwa zinasubiriwa ili kuanza shughuli.
Ufadhili huu unajumuisha shughuli zinazohusiana na uimarishaji na ujumuishaji wa jamii pamoja na ugatuzi wa utawala. Benki ya dunia imesema ruzuku zitatekelezwa katika majimbo hayo na kwamba lengo ni kujaribu kuimarisha shughuli za upokonyaji silaha ambazo hazikufaulu hapo awali.
Kwa hakika, mpango huo utajaribu kuzuia vijana kujiunga na makundi yenye silaha, na pia utajihusisha na wapiganaji wa zamani waliojisalimisha ili kujua wanawezaje kufalia jamii zao.
Mwaka jana, mamia ya wapiganaji waliojisalimisha na kuweka silaha chini wamerejea tena msituni haswa katika majimbo ya Kivu kusini na Kivu kaskazini kwa kukosewa na huduma muhimu. Wataalamu wa masuala ya kiusalama wamesema wapiganaji hao wamerudi msituni kufuatia ukosefu wa mtazamo na miradi ya upokonyaji silaha iliyofafanuliwa wazi na serikali na washirika wake. Augustin Ntayitunda ni mchambuzi wa masuala ya kiusalama Kivu kusini, anahisi kwamba licha ya ufadhili huo, huenda utekelezwaji wa mpango huo utakuwa na changamoto fulani:
Usaidizi huo wa benki ya dunia unahusu pia utoaji wa ruzuku ndogo ndogo katika ngazi za kijamii ukiambatana na shughuli za kuzalisha mapato. Sehemu ya fedha hizo pia itachangia kwa usaidizi wa kisaikolojia na huduma za afya ya akili kwa wapiganaji hao na pia wahanga wa athari mbalimbali za kivita katika jamii, na sehemu nyingine itasaidia kufanikisha shughuli za uhamasishaji ili kuzuia na kudhibiti migogoro.
Mwaka wote mzima uliopita mpango wa serikali ya Congo wa kupokonya silaha PDDRC-S umeunda mikakati muhimu ili kufanikisha upokonyaji huo. Washirika wa kimataifa kama vile Umoja wa Ulaya na Benki ya Dunia walikuwa bado wanasubiri kuwasilishwa kwa mpango wa kina. Miongoni mwa masharti waliyoweka ya kufadhili programu hii ni uundwaji mkakati unoaminika na uliofafanuliwa wazi kuhusu utekelezwaji wa mpango huo.
Mitima Delachance, DW, Bukavu