Berlin.Mawaziri wa Ujerumani wakana kufahamu kuhusu kukamatwa kwa raia wa Kijerumani na CIA.
15 Desemba 2006Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na mtangulizi wake Joschka Fischer wamekana kuwa walikuwa wanafahamu madai ya kukamatwa raia mmoja wa Ujerumani na makachero wa shirika la ujasusi la Marekani CIA. Viongozi hao wote wawili wameuambia uchunguzi wa bunge kuwa madai hayo hayana msingi. Khaled el Masri , raia wa Ujerumani mwenye asili ya Lebanon , alikamatwa nchini Macedonia mwishoni mwa mwaka 2003 na amesema kuwa alifungwa na CIA kwa muda wa miezi kadha nchini Afghanistan kabla ya kuachiliwa huru mwaka 2004. wakati huo Fischer alikuwa waziri wa mambo ya kigeni wakati Steinmeier alikuwa msaidizi mwandamizi wa kansela wa zamani Gerhard Schroeder. Vyombo vya habari vya Ujerumani vimesema kuwa Steinmeier alipata taarifa juu ya kukamatwa kwa el Masri na CIA mapema Januari 2005 , lakini alishindwa kuiarifu kamati ya udhibiti ya bunge.