Bi Clinton atoa nasaha kabla ya kuondoka
1 Februari 2013Katika mkutano na kundi dogo la waandishi wa habari pamoja na wanadiplomasia wa ngazi ya juu hapo jana, Hillary Clinton alielezea kwa mukhtasari masuala ambayo mtu anayechukua wadhifa wake, John Kerry atayakuta mezani atakapoanza kazi rasmi Jumatatu ijayo.
Lakini alianza na hatua iliyopigwa wakati akiwa mkuu wa diplomasia ya Marekani chini ya uongozi wa rais Barack Obama, yakiwemo kumalizika kwa vita vya Irak, kuuawa kwa kiongozi wa al-Qaida Osama bin Laden, na kuunda ushirika imara na washirika wa Marekani kote duniani.
Dira mpya ya kidiplomasia
Akizungumzia dira ya Mrekani katika uwanja wa kimataifa, Hillary Clinton alisema inabidi nchi hiyo itumia vizuri uwezo wake.
''Tunapaswa kuwa waerevu katika kutumia raslimali zetu. Licha upungufu katika bajeti, nguvu za jeshi letu, uwezo wetu kiuchumi, na ushawishi wa kidiplomasia, vimekuwa bora zaidi. Hii ni kwa sababu dunia imebadilika, sambamba na vigezo vingine vinavyoweza kushawishi mwelekeo wa matukio duniani.'' Alisema Clinton.
Bi Clinton aliitaja vita inayoendelea nchini Syria, na kuielezea kama mgogoro unaozua wasiwasi mkubwa, na ambao unatabiriwa kuwa na athari mbaya kabisa ndani ya Syria yenyewe, na vile vile nje ya mipaka ya nchi hiyo, akiongezea kuwa ni suala linalopaswa kuangaliwa kwa makini. Alizishutumu Iran na Urusi kuendelea kuisaidia serikali ya Rais Bashar al-Assad, kwa kuipatia fedha na silaha.
Mizozo chungu nzima
Kuhusu mzozo juu ya mpango wa nyuklia wa Iran, Bi Clinton alisema kuwa ingawa Marekani ilitaka mzozo huo umalizike kwa njia ya mazungumzo, muda wa majadiliano hauwezi kuwepo milele. Hakusema ni muda gani unaobakia kuendelea na mazungumzo hao, lakini alisema bila shaka mlango wa mazungumzo hauwezi kubaki wazi kwa muda mrefu.
Mgogoro mwingine ambao Bi Clinton alisema John Kerry atapaswa kuuangalia mara tu atakapoanza kazi, ni ule wa Korea Kaskazini. Alisema Marekani iliwahi kuamini kuwa ilikuwa ikipata maelewano na aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo
Kim Jong Il, lakini kiongozi huyo alifariki na nafasi yake ikachukuliwa na mwanae, ambaye bado Marekani na Washirika wake wanahitaji muda wa kumfahamu vizuri.
Sifa za ufanisi
Kuhusu Afghanistan, Hillary Clinton alitilia mkazo suala la haki za wanawake, na kusisitiza kuwa Marekani haina budi kuendelea kuziunga mkono taasisi zinazotetea haki sawa za wanawake nchini Afghanistan, baada ya vikosi vya kimataifa kuondoka nchini humo mwaka Ujao.
Mambo mengine ambayo waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Marekani anayeondoka alisema yanahitaji kuangaliwa kwa makini na mrithi wake, ni mashambulizi ya kimtandao yanayoongezeka, kitisho cha ugaidi katika kanda ya Afrika Kaskazini.
Wachambuzi wengi wanamsifu Hillary Clinton kwa namna alivyotekeleza majukumu yake kama waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, hususan katika kuirejeshea marekani sura nzuri kwenye uwanja wa kimataifa, na kurudisha hali ya kushirikiana na washirika wake katika majukumu ya kimataifa.
Mwandishi: Daniel Gakuba/dpa/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef