1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biashara ya silaha ya Ujerumani kwa Saudi Arabia Magazetini

Oumilkheir Hamidou
2 Oktoba 2018

Biashara ya silaha za Ujerumani kwa Saudi Arabia, kukamatwa watuhumiwa sita wa siasa kali za mrengo wa kulia mjini Chemnitz na miaka 28 ya muungano ni miongoni mwa mada magazetini.

https://p.dw.com/p/35r9U
Deutschland Oberndorf am Neckar Staffellauf nach Berlin gegen Rüstungsexporte
Picha: picture-alliance/dpa/S. Schmidt

Tunaanzia Berlin ambako biashara ya silaha ya Ujerumani kwa Saudi Arabia inakosolewa mtindo mmoja na wahariri. Mhariri wa gazeti la "Oberhessische Presse" anasema biashara hiyo haistahiki: "Tangu marchi serikali kuu ya Ujerumani imeiuzia Saudi Arabia silaha zenye thamani ya Euro milioni 254 pamoja na kujikusanyia Euro milioni 21.8 kutokana na biashara kama hiyo katika nchi zinazoshirikiana na Saud Arabia. Mhariri wa Oberhessische Presse anajiuliza ndo kusema serikali kuu ya Ujerumani haijui kama Yemen kuna vita. Biashara hiyo haihalaliki, seuze tena nafasi chini ya laki moja za kazi katika viwanda vya silaha haziwezi kulinganishwa na maisha ya malaki ya watoto wanaouliwa nchini Yemen."

Wafuai wa siasa kali za mrengo wa kulia wakamatwa kwa kuandaa njama ya hatari

 Kwa mujibu wafisi ya mwendesha mashitaka mkuu mjini Karlsruhe watuhumiwa sita wa kundi la siasa kali za mrengo wa kulia wamekamatwa mjini Chemnitz. Walilenga kufanya shambulio kubwa Oktoba  tatu, siku ya muungano, wakiwalenga tangu wageni mpaka viongozi wa kisiasa na kijamii. Gazeti la "Merkische Oderzeitung" linaandika:" Mara nyingi idara za usalama zimekuwa zikituhumiwa, na si bure, kwamba wanapenda kufumba jicho la kulia. Kwa hivyo ni vyema kuwaona katika kadhia hii wameyafumbua yote mawili.Yeyote anaetaka kutumia nguvu dhidi ya msingi wa kuishi pamoja raia, anadhamiria kuivuruga jamii. Na hapo hatua kali tu ndio dawa."

Nalo gazeti la mjini Cologne,"Kölner Stadt Anzeiger" linatahadharisha: "Ni hatari kuleta uwiano wa visa vya makundi tofauti ya siasa kali. Huwezi kwa mfano panapotokea shambulio la kigaidi la mrengo wa kulia kuleta uwiano na shambulio la makundi ya mrengo wa kushoto au kupunguza matumizi ya kuwapeleleza  wanazi kwaajili ya kuwaajiri wataalam zaidi wa itikadi kali. Ikiwa Saxony na wanasiasa wake wanataka kuondokana na sifa mbaya ya kuitwa ngome ya mashariki ya wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia, wanahitaji kitu kimoja tu,  kuwatenga moja kwa moja wafuasi wake."

Miaka 28 ya Muungano wa Ujerumani

Na hatimae  gazeti la "Südwest" linazungumzia miaka 28 ya muungano. Gazeti linaandika: "Ni kweli kabisa wengi walikuwa na mitazamo tofauti October tatu mwaka 1990. Licha ya yote  kuna  cha muhimu kilichopatikana. Na tangu lini mambo yakafanikiwa mia kwa mia? Ikilinganishwa na kwengineko, basi wajerumani wana raha.Tofauti zilizoko kati ya mashariki na magharibi si chochote ikilinganishwa na majanga mengine yanayoshuhudiwa katika sayari yetu."

 

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman