Biashara ya silaha yapungua kidogo
18 Februari 2013Tuanzie na ripoti ya taasisi ya kimataifa ya SIPRI inayozungumzia jinsi biashara ya silaha ilivyopungua. Sababu ripoti hiyo inasema ni mgogoro wa kiuchumi. "Landeszeitung" linaandika:
Makasha matupu ya serikali yamevifanya viwanda vya silaha kuondoka patupu. Lakini furaha ya wapenda amani iliyosababishwa na tarakimu mpya za taasisi ya SIPRI ni ya bure. Kwa sababu kwa jumla biashara ya silaha haionyeshi kwamba imetuwama seuze kupungua. Kuna hali mbili tofauti zilizojitokeza katika sehemu mbili za dunia yetu. Asia inaendelea kujirundikia silaha, Ulaya inapunguza. Yadhihirika kana kwamba hali ya siku za mbele itakuwa pia tofauti kati ya pande hizi mbili za dunia. Katika wakati ambapo Ulaya inajihadaa na kufikiria kwamba ulimwengu ni sawa na Umoja mpana wa Ulaya, suala la masilahi ya kula upande linaweza kufumbuliwa kwa njia ya mazungumzo na kusambazwa hundi, bara la Asia linajirundikizia silaha tayari kwa mapambano ya kuania uamuzi.
Umaskini katika jamii
Hali ya umaskini miongoni mwa wahamiaji ni mada nyengine iliyochambuliwa na wahariri. Gazeti la "Straubinger Tagblatt / Landshuter Zeitung linaandika:"Wasiwasi ni mkubwa katika maeneo husika. Wenyeji mara nyingi wanaghadhibika, wanahamaki na hata kuchukizwa na kelele zinazohanikiza, vitu vinavyoharibiwa na matukio mengine ambayo kawaida hujitokeza watu wanapoishi pamoja kama majirani. Hali hiyo inasababisha hisia za chuki. Hata Umoja wa Ulaya unatiwa hatiani. Serikali kuu ya Ujerumani inabidi ishinikize mjini Brussels ili hali mbaya ya kiuchumi na kijamii katika nchi watu wanakotokea iimarishwe kwa namna ambayo watu hao wasitamani tena kuzihama nchi zao na kuelekea Ujerumani au nchi nyengine za Umoja wa Ulaya. Wanahitaji kuwa na matumaini mema ya maisha katika nchi wanakotokea.
Wanunuzi mashakani
Ripoti yetu ya mwisho inahusu kashfa ya nyama ya farasi. Kashfa hiyo iliyoanzia katika chakula cha Lasagne ambacho kawaida kutengenezwa kwa nyama ya ngome inaonyesha kuenea katika vyakula vyengine na katika nchi tofauti za Ulaya. Gazeti la General Anzeiger la mjini Bonn linaandika:Ndio uchunguzi wa kina zaidi ni muhimu lakini pia adhabu kali zaidi zinahitajika. Tunahitaji hivi sasa wanasiasa ambao, kinyume na yule wa chama cha walinzi wa mazingira katika jimbo la North Rhine Westfalia anayeshughulikia kinga ya wanunuzi, hatotoa hutuba tupu tu, badala yake atachukua hatua zinazostahiki. Kuchunguzwa vyakula ni jukumu la serikali za majimbo. Na ni suala linalohusu masilahi ya wanunuzi. Anayenunua chakula safi cha mkoani, na kukitengeneza mwenyewe, hawezi kukabiliwa na hatari ya udanganyifu.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Josephat Charo