1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden aondoka kuelekea Ulaya

23 Machi 2022

Rais Joe Biden wa Marekani ameondoka mjini Washington kuanza ziara ya siku nne barani Ulaya, ambako anatarajiwa kukutana na washirika muhimu kujadiliana juu ya uvamizi wa urusi nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/48wQX
Joe Biden zum Gesetz gegen Gewalt an Frauen
Picha: Tom Brenner/REUTERS

Kwenye ziara hiyo rais Joe Biden pamoja na mambo mengine atahuhduria mikutano ya Umoja wa Ulaya na kundi la mataifa saba tajiri zaidi ulimwenguni la G7, lakini pia atakutana na maafisa wa ngazi za juu wa Poland, inayopakana na Ukraine. 

Alipokuwa akiondoka Washington, Biden aliwaambia waandishi wa habari kuhusu uwezekano wa Urusi kutumia silaha za kemikali katika vita nchini Ukraine, akisema hicho ni kitisho cha dhahiri. Akasema atalizungumzia kwa kina hilo atakapokutana na viongozi wenzake kwenye ziara hiyo.

Soma zaidi: Biden adai Urusi inakusudia kutumia silaha za kemikali

Ziara yake itaanzia Brussels, makao makuu ya Umoja wa ulaya ambako atahudhuria mkutano wa dharura wa kilele wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, na baadaye atahudhuria mikutano ya Umoja wa Ulaya na kundi la G7, linalojumuisha mataifa saba tajiri zaidi ulimwenguni. Na siku ya Ijumaa, Biden atakwenda Poland na huko atakutana na maafisa wa ngazi za juu ikiwa ni pamoja na rais Andrej Duda.

Mapema leo katibu mkuu wa muungano huo wa NATO Jens Stoltenberg ametangaza kwamba watapeleka wanajeshi katika maeneo ya Bulgaria, Hungary, Romania na Slovakia.

Japan | Video-Übertragung Rede Wolodymyr Selenskyj vor dem Parlament in Tokio
Rais Volodymyr Zelensky akilihutubia bunge la Japan na kuiomba kuongeza mbinyo dhidi ya UrusiPicha: Kazuhiro Nogi/AFP/Getty Images

Huko Japan, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amelihutubia bunge la nchi hiyo akianza kwa kulipongeza kuwa taifa la kwanza barani Asia kuweka mbinyo dhidi ya Urusi huku akilitolea mwito kuongeza vikwazo, lakini kwa upande mwingine akielezea wasiwasi wake kwamba jirani yake huyo huenda akatumia silaha za kemikali.

"Kinu cha nyuklia cha Chernobyl kimeangukia kwenye udhibiti wa Urusi ambayo imekigeuza na kuwa uwanja wa vita. Itachukua miaka mingi kutathmini kiwango cha uharibifu wa mazingira baada ya vita hivi kumalizika. Nimepata ripoti kwamba Urusi inajiandaa kufanya mashambulizi yanayohusisha silaha za kemikali kama ya sarin kama walivyofanya Syria. Imekuwa ikijadiliwa namna ulimwegu utakavyojibu iwapo silaha za nyuklia zitatumika," alisema Zelensky.

Rais Vladimir Putin asema pamoja na vikwazo wataendelea kuuza gesi kama kawaida.

Katika mji wa Vatican, kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis kwa mara nyingine ameombea amani nchini Ukraine huku akiongeza matamshi binafsi yanayoelezea chuki yake dhidi ya vita. Papa Francis aliwaombea wahanga wa uvamizi wa urusi nchini Ukraine ikiwa ni pamoja na wanajeshi wengi waliokufa kutoka pande zote. Amezitolea mwito serikali kutambu kwamba kununua na kuzalisha silaha kamwe hakuwezi kuwa suluhu.

Katika hatua nyingine, Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema leo kwamba Urusi itaanza kuyauzia gesi mataifa yasiyo marafiki zake, kufuatia hatua ya mataifa ya magharibi ya kuzuia mali za Urusi ambayo inasema imeondoa uaminifu wake kwa mataifa hayo.

Amesema kupitia hotuba iliyorushwa kwenye televisheni kwamba Urusi itaendelea kusambaza gesi asilia katika kiwango na bei ileile ya awali iliyofikiwa kwenye mikataba. Alikuwa akizungumza na mawaziri wa serikali yake na kuongeza kuwa kitakachobadilika ni sarafu itakayotumiwa kulipia ambayo sasa itakuwa ni ya Urusi.

Mashirika: DW/RTRE/APE