Biden asema Netanyahu anakwamisha mapatano Gaza
2 Septemba 2024Rais Joe Biden wa Marekani amesema hii leo kwamba anakaribia kuwasilisha pendekezo la mwisho la makubaliano ya kuachiliwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza na kusema hadhani kama Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anafanya vya kutosha kufikia makubaliano hayo.
Biden alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House siku mbili baada ya vikosi vya Israel kusema vimegundua miili sita ya mateka kwenye handaki huko Gaza.
Soma pia: Hamas yasema Biden anaipa Israel "Tiketi" ya kuendeleza vita
Kupatikana miili hiyo kumeibua ukosoaji zaidi dhidi ya mpango wa Biden wa kusitisha mapigano katikati ya kampeni za urais nchini Marekani na kuongeza shinikizo dhidi ya Netanyahu kutoka kwa Waisraeli wanaomtaka kuwarejesha mateka nyumbani.
Ukosoaji huu mpya wa Biden dhidi ya Netanyahu unakuja wakati yeye na makamu wake Kamala Harris anayewania urais katika uchaguzi wa mwezi ujao pia wakikabiliwa na ongezeko la miito ya hatua kali katika kuumaliza mzozo huo uliodumu kwa miezi 11.