Biden ataka silaha za mashambulizi zipigwe marufuku
3 Juni 2022Akizungumza Alhamisi katika Ikulu ya Marekani kuhusu mashambulizi ya kutumia bunduki, Biden amesema maeneo mengi ya Marekani kila siku yamekuwa maeneo ya mauaji. Biden amebainisha kuwa hakuna chochote kilichofanywa baada ya mauaji ya watu wengi kwa kutumia bunduki, lakini wakati huu lazima wachukue hatua. Amesema umri wa mtu kununua silaha unapaswa kuongezwa na pia wanatakiwa kupiga marufuku silaha za mashambulizi.
''Na kama hatuwezi kupiga marufuku silaha za mashambulizi, basi tunapaswa kuongeza umri wa mtu anaoruhusiwa kununua silaha kutoka miaka 18 hadi 21, kuangalia historia yake, kuondoa kinga inayowalinda watengenezaji wa bunduki kuwajibika kisheria, tuzungumzie afya ya akili. Hizi ni hatua za kawaida,'' alifafanua Biden.
Biden ataka mbadiliko kwenye baadhi ya sheria za silaha
Kiongozi huyo wa Marekani amerudia wito wa serikali yake kuhusu kuifanyia marekebisho Sheria ya Ulinzi wa Biashara Halali ya Silaha, ambayo inazuia wanaotengenza bunduki kuwajibishwa kwa uhalifu unaofanywa kutokana na bidhaa zao. Biden aliuliza ni mauaji kiasi gani zaidi yatokee ndiyo wataweza kukubaliana na hali halisi?
Biden amesema ameshangazwa na hatua ya wabunge wengi wa chama cha Republican katika Baraza la Seneti kukataa kuchukua hatua yoyote kuhusu sheria inayohusu mashambulizi ya kutumia bunduki na umiliki wa bunduki, akisema hatua hiyo haina maana.
Biden amewataka wabunge kupiga marufuku matumizi ya silaha zinazomilikiwa na watu binafsi ili kukabiliana na mauaji ya watu wengi yanayolikumba taifa hilo. Amebainisha kuwa sheria kama hizo zingeweza kuzuia baadhi ya mauaji ya risasi yaliyotokea hivi karibuni nchini humo.
Wanachama wa Republican wapinga muswada wa kumiliki silaha
Wabunge wa Republican hata hivyo, wamepinga jaribio la wabunge wa chama cha Democratic kuweka taratibu mpya kuhusu manunuzi ya bunduki. Muswada huo utaongeza umri wa chini kwa mtu kuruhusiwa kununua silaha kutoka miaka 18 hadi 21 na kupunguza ulanguzi wa silaha.
Wabunge wa chama cha Biden cha Democratic wanahitaji kuungwa mkono na baadhi ya wabunge wa Republican ili kuipitisha sheria hiyo ya udhibiti wa bunduki. Muswada huo unahitaji kura 60 kati ya 100 ili uweze kupita, hatua inayomaanisha kwa muundo wa sasa wa Baraza la Seneti, sheria yoyote mpya itahitaji kuungwa mkono na baadhi ya wabunge wa Republican.
Kuongezeka kwa mauaji ya kufyatuliana risasi ya hivi karibuni kumezusha mjadala wa udhibiti wa silaha nchini Marekani. Mapema wiki hii, mwanaume aliyekuwa na bunduki aliingia katika kituo cha afya huko Tulsa, Oklahama na kuwaua watu wanne. Wiki iliyopita, mwanaume mwenye silaha aliwaua watoto 19 na walimu wawili katika shule ya msingi huko Uvalde, Taxas. Mapema mwezi Mei, mtu aliyefyatua risasi aliwaua watu 10 katika duka moja kubwa huko New York. Baada ya mauaji hayo, Rais Biden aliahidi kukutana na Bunge kujadiliana kuhusu sheria za umiliki wa bunduki.
(AP, AFP Reuters)