1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden atishia kumwekea Putin vikwazo binafsi

26 Januari 2022

Rais wa Marekani Joe Biden amesema huenda Marekani ikamwekea rais wa Urusi Vladimir Putin vikwazo binafsi ikiwa Urusi itaivamia Ukraine.

https://p.dw.com/p/465Xe
Washington US Präsident Joe Biden
Picha: Leah Millis/REUTERS

Joe Biden alipoulizwa na mwandishi wa Habari ikiwa anaweza kufanya uamuzi wake mwenyewe kumwekea Putin vikwazo binafsi, alijibu kwa kusema- ndiyo.

Jibu lake lilijiri mnamo wakati vikosi vya Urusi vikianza mazoezi mapya ya kijeshi karibu na Ukraine.

Urusi: Marekani inachochea mzozo wa Ukraine

Biden alisema ikiwa Urusi itafanya uvamizi nchini Ukraine, basi unaweza kuwa uvamizi mkubwa zaidi kuwahi kufanyika tangu Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na utabadili ulimwengu.

Ujerumani yaitaka Urusi kuondoa wasiwasi uliopo

Emmanuel Macron (kushoto) na mwenyeji wake Olaf Scholz wa Ujerumani wakizungumza na waandishi habari Berlin baada ya mkutano wao ambapo walijadili pia mzozo wa Ukraine.
Emmanuel Macron (kushoto) na mwenyeji wake Olaf Scholz wa Ujerumani wakizungumza na waandishi habari Berlin baada ya mkutano wao ambapo walijadili pia mzozo wa Ukraine.Picha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Wakati huo huo kansela wa Ujerumani Olaf Scholz pia ametoa onyo kwa Urusi kuwa itaadhibiwa ikiwa itavamia Ukraine. 

Marekani, EU wajadili jibu la pamoja kwa Urusi kuhusu mzozo wa Ukraine

Onyo la Olaf Schol limejiri baada ya mkutano wake na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron mjini Berlin Jumanne ambapo walijadili mzozo huo wa Ukraine pamoja na masuala mengine.

Scholz amesema hali ni ngumu katika mpaka wa Ukraine na Urusi ambapo Urusi imewarundika takriban wanajeshi wake 100,000.

"Tunatarajia Urusi itachukua hatua za kweli za kupunguza mivutano iliyopo na tumekubaliana sote kwamba uchokozi wa kijeshi utajibiwa kwa kali,” amesema Scholz.

Wachambuzi waamini Urusi hailengi kufanya uvamizi

Kwa upande wake rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema atapendekeza mpango kwa rais wa Urusi Vladimir Putin wa kuondoa wasiwasi uliopo katika mkutano wao siku ya Ijumaa.

Kuna wasiwasi miongoni mwa nchi za magharibi kwamba huenda Urusi inapanga kuivamia Ukraine.

Hata hivyo wachambuzi wengi wanaamini kwamba Urusi inajitutumua tu ikiwa ni lengo lake la kuzuia jumuiya ya kujihami ya NATO kusogea karibu na mipaka yake na kushinda dhamira ya makubaliano yake mapoya ya kiusalama.

Mnamo Jumatatu wizara ya Ulinzi ya Marekani iliwaamuru wanajeshi wake 8,500 kuwa tayari kupelekwa Ulaya kuwa sehemu ya NATO kujibu uvamizi wowote utakaofanywa na Urusi.

Urusi imewarundika wanajeshi wake karibu na mpaka wake na Ukraine, hatua inayohofiwa kuwa kitisho cha kutaka kuivamia Ukraine.
Urusi imewarundika wanajeshi wake karibu na mpaka wake na Ukraine, hatua inayohofiwa kuwa kitisho cha kutaka kuivamia Ukraine.Picha: Russian Defense Ministry Press Service/AP/dpa/picture alliance

Wawakilishi wa Urusi na Ukraine kukutana kwa mara ya kwanza

Katika juhudi zinazoendelea kutafuta suluhisho la kidiplomasia kuhusu mgogoro huo, wawakilishi wa Ukraine na Urusi wanatarajiwa kukutana leo kwa mara ya kwanza tangu mzozo huo kuanza mwaka uliopita.

Sintofahamu yaendelea kugubika mazungumzo kuhusu Ukraine

Mkutano huo utakaofanyika Paris utawaleta Pamoja washauri wa kisiasa kutoka nchi nne ikiwemo Ujerumani na Ufaransa.

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine amesema lengo la Urusi ni kueneza wasiwasi.

(DPA, RTR, AP)