Biden autembelea mradi wa reli Angola
4 Desemba 2024Rais wa Marekani Joe Biden yuko nchini Angola katika siku yake ya mwisho ya ziara ya siku tatu na ameutembelea mradi mkubwa wa miundombinu ya reli unaofadhiliwa na nchi yake unaofahamika kama Ukanda wa Lobito. Mradi huo unahusisha ukarabati wa kiasi kilometa 1,300 za njia ya reli inayoziunganisha nchi tatu za Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Angola hadi kwenye bandari ya Lobito iliyopo kwenye fuo za bahari ya Atlantiki.
Zikiwa zimbaki siku chache katika kiti cha Urais wa Marekani, Rais Joe Biden yuko nchini Angola katika ziara ya kihistoria akiutembelea mradi mkubwa wa reli nchini humo.
Soma zaidi. Biden azuru mradi wa reli nchini Angola, anapomalizia ziara
Biden ametumia siku yake ya tatu na ya mwisho katika ziara yake kuutembelea mradi wa reli ya Lobito ambapo nchi yake ya Marekani na washirika wake zimewekeza katika ukarabati wa mradi huo mkubwa wa reli wenye kilomita 1,300 ambao unaziunganisha nchi za Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Angola.
Mradi huo unalenga kuendeleza uwepo na ushawishi wa Marekani katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa kobalti, shaba na madini mengine muhimu yanayotumika kwenye betri magari ya umeme, vifaa vya kielektroniki na teknolojia ya nishati safi.
Mwishoni mwa muongo huu, njia hiyo ya reli inaweza kurefuka zaidi na kwenda mbali na kuunganisha pwani ya kusini magharibi na eneo la mashariki mwa Afrika.
Soma zaidi. Rais Joe Biden aahidi ushirikiano wa kudumu baina ya Marekani na Afrika
Mapema hii leo, Biden alisafiri kwa ndege kutoka mji mkuu wa Angola wa Luanda hadi Lobito kwenye pwani ya magharibi ya nchi hiyo ma kutembelea eneo hilo la bandari akiwa na mwenyeji wake Rais waAngola João Lourenço, Rais wa Zambia Hakainde Hichilema, Rais wa Kongo Felix Tshisekedi na Makamu wa Rais wa Tanzania Philip Mpango.
Viongozi hao watakutana pia na wawakilishi wa makampuni mbalimbali yanayotarajiwa kufanya biashara kupitia mradi huo ikiwemo makampuni ya simu, makampuni ya mazao na yale ya ujenzi nchini Angola.
Mradi huu utaongeza ushawishi wa Marekani barani Afrika
Utawala wa Biden unasema mradi huo wa reli utasaidia kuongeza maslahi ya biashara huku ukilenga pia kukabiliana na ushawishi wa China unaokua barani Afrika. Mradi huo ni mpango wa muda mrefu ambao ulisubiriwa kwa miaka mingi hasa wakati ambapo mvutano wa kibiashara kati ya China kuhusu madini yanayohitajika kwenye teknolojia ukizidi kuongezeka.
Biden atatangaza pia dola milioni 600 ambazo zitatumika katika miradi inayoendana na mradi huo wa reli, pesa ambazo zinafadhiliwa pia na Umoja wa Ulaya,mataifa yaliyoendelea kiviwanda na baadhi ya benki za afrika.
Soma zaidi. Hatimaye Biden awasili Angola
Kwa upande mwingine, China yenyewe tayari ina uwekezaji mkubwa katika madini na usindikaji wa madini ya kutoka Afrika ambapo inatumia mpango wake wa ujenzi wa miundombinu kuongeza ushawishi duniani.
Mfano, Mwezi Septemba, China ilisema kuwa imesaini mkataba na Tanzania na Zambia wa kurekebisha njia ya reli inayoenda mashariki kutoka Zambia hadi Dar es Salaam ya Tanzania.