1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden azidi kupongezwa

9 Novemba 2020

Rais mteule wa Marekani Joe Biden ameendelea kupongezwa huku viongozi wengi wakiwa na matumaini na nia ya kushirikiana na kiongozi huyo baada ya miaka kadhaa ya mivutano na chini ya utawala wa rais Donald Trump.

https://p.dw.com/p/3l2po
USA Wilmington | Rede Joe Biden und Kamala Harris nach dem Wahlsieg
Picha: Andrew Harnik/AP Photo/picture alliance

Ulimwengu umeendelea kutuma salamu za pongezi kwa rais mteule wa Marekani Joe Biden huku viongozi wengi wakionyesha matumaini na nia ya kushirikiana kwa karibu na kiongozi huyo baada ya miaka kadhaa ya mivutano na sintofahamu chini ya utawala wa rais Donald Trump. Hata hivyo wapo baadhi wanaosema bado ni mapema mno kumpongeza rais huyo mteule. 

Makundi yanayoiunga mkono Iran yaliyoko nchini Iraq yameukaribisha ushindi wa Joe Biden hali inayowatia wasiwasi maafisa na wanaharakati mjini Baghdad wanaohofia kwamba mzozo kati ya Iran na Marekani huenda ukayaimarisha makundi yenye misimamo mikali ndani ya nchi yao.

Baghdad kwa muda mrefu imejikuta katika mvutano mkali wa kiushawishi kati ya washirika wake hao wawili, Washington na Tehran ambao ulichochewa hata zaidi na shinikizo kubwa kufuatia kampeni ya rais anayeondoka madarakani Donald Trump dhidi ya Iran tangu mwaka 2018.

Makundi yanayohasimiana nchini Iraq na yanayoungwa mkono na Tehran yana matumaini kwamba Biden atabadilisha sera ya Trump, ambazo ni pamoja na kuyafyatulia mabomu makundi yenye misimamo mikali na kuwawekea vikwazo vikali wanaoiunga mkono Iran.

Irak Baghdad Schiiten-Miliz Ketaeb Hezbollah
Wanamgambo wa kundi la Ketaeb Hezbollah ni miongoni mwa makundi yenye matarajio makubwa na BidenPicha: Getty Images/AFP/S. Arar

Msemaji wa kundi la Kataeb Hezbollah Mohammad Mohyi amesema wana matumaini serikali mpya itasuluhisha hayo yote, huku akiungwa mkono na Khamees al-Khanjar kiongozi wa madhehebu ya Sunni na mwenye ushawishi mkubwa aliyesema ushindi wa Biden ni fursa mpya na Marekani kuelekea sura ya kimataifa, lakini pia utakaofungua ukurasa mpya kuelekea ustahimilivu na mazungumzo.

Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in alipompongeza Biden hii leo amesema nchi yake itahakikisha hakutokei pengo la kimahusiano na Marekani lakini pia kuimarisha mchakato wa kuhakikisha amani kwenye rasi ya Korea. Korea Kusini inamchukulia Trump kama mshirika katika juhudi za kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, lakini mahusiano yao yaliingia doa kufuatia kutokukubaliana juu ya namna ya kukubaliana na Korea Kaskazini, biashara na shinikizo la Trump kwa Korea Kusini la kulipa mabilioni zaidi ya dola kuvisaidia vikosi vya Marekani vilivyoko kwenye rasi hiyo. 

Russland Moskau | Russische Sicherheitsratssitzung | Wladimir Putin
Rais Vladimir Putin bado hajasema chochote kuhusu ushindi wa Joe BidenPicha: Alexei Druzhinin/dpa/picture-alliance

Hata hivyo, baadhi ya wakuu wa nchi wamekataa kumpongeza rais huyo mteule moja kwa moja. Ikulu ya Kremlin ya Urusi imesema hii leo kwamba itasubiri matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais, lakini pia imesema inazingatia tangazo la Donald Trump la kuyapinga matokeo mahakamani. Rais Vladmir Putin amesalia kimya tangu Biden alipoonekana kushinda siku ya Jumamosi.

Akizungumza na waandishi wa habari msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov amesema mjini Moscow kwamba ni vyema kusubiri matokeo rasmi na kuongeza kuwa tayari rais Putin mara kwadhaa amesema yupo tayari kushirikiana na rais yoyote wa Marekani na matumaini ya kuanzisha majadiliano ya kusaka suluhu ya ushirikiano baina yao.

China nayo imesema itafuata taratibu za kimataifa katika kutoa taarifa kuhusiana na uchaguzi huo. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Wang Wenbin amewaambia wana habari kwamba wanatambua kwamba Biden ametangaza kushinda na kusema wanajua kwamba matokeo rasmi yatazingatia misingi ya sheria za taifa hilo.

Soma Zaidi: Biden anaweza kurudisha ushirikiano wa kimataifa na uongozi?

Mashirika: AFPE/RTRE