Blinken afanya mazungumzo ya faragha na mwenzake wa Uturuki
6 Novemba 2023Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amefanya mazungumzo ya faragha leo Jumatatu na mwenzake wa Uturuki Hakan Fidan mjini Ankara kujaribu kutuliza hasira za nchi hiyoambayo ni mmoja wa washirika wake muhimu wa kimkakati.
Ziara ya Blinken Uturuki ni ya kwanza nchini humo tangu Israel ilipoingia vitani na kundi la Hamas kujibu mashambulizi yaliyofanywa Oktoba 7 na kundi hilo katika ardhi ya Israel.
Polisi walitumia gesi ya kutowa machozi na mabomba ya maji dhidi ya umma wa mamia ya watu walioandamana katika kambi ya jeshi la wanaanga la Marekani Kusini Mashariki mwa Uturuki, saa chache kabla ya Blinken kuwasili jana Jumapili.
Soma pia:Blinken afanya ziara ya kushtukiza Ukingo wa Magharibi
Rais Recep Tayyip Erdogan amekwenda kulitembelea eneo la Kaskazini Mashariki mwa nchi yake hii leo katika hatua inayoonekana ni ya kumpuuza mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Marekani.
Vita vya Gaza vinatishia kuhatarisha mahusiano ya Marekani na Uturuki ambaye ni mwanachama wa Nato na ambayo ina ushawishi mkubwa katika migogoro ya eneo zima la Mashariki ya Kati.