1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken akutana na El-Sisi kujadili mzozo wa Gaza

6 Februari 2024

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amekutana na Rais wa Misri Abdel Fattah El-sisi kama sehemu ya kutafuta makubaliano ya kusitisha vita kati ya Israel na Hamas.

https://p.dw.com/p/4c6U9
Misri Cairo | Antony Blinken na rais Abdel Fattah El-sisi
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alipokutana na Rais wa Misri Abdel Fattah El-sisi mjini Cairo.Picha: Jacquelyn Martin/REUTERS

Blinken amewasili Misri baada ya kuitembelea Saudi Arabia na baadaye ataelekea Qatar. Nchi hizo mbili zimechukua jukumu la kuwa wapatanishi katika vita kati ya Israel na Hamas.

Marekani kwa wiki kadhaa sasa imekuwa ikitafuta makubaliano ya kuachiliwa huru mateka waliosalia kwa mabadilishano ya kuwepo kwa usitishaji wa muda mrefu wa vita vinavyoendelea.

Hata hivyo, hakukuwepo tamko lolote kutoka upande wowote kuhusu iwapo mazungumzo ya Blinken mjini Riyadh na Cairo yalikuwa na mafanikio.

Afisa wa kundi la Hamas ambaye hakutaka jina lake litajwe, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa kundi hilo halitobadilisha msimamo wake wa kutoachilia huru mateka hadi pale vita vitakapositishwa na vikosi vya Israel kuondoka Gaza.