1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken: Urusi ikithubutu kuingia Ukraine itakabiliwa

20 Januari 2022

Umoja wa Ulaya umetishia kuiwekea vikwazo Urusi ikiivamia Ukraine na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken amekutana na marafiki wa Marekani kuelekea mkutano na Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov.

https://p.dw.com/p/45qY9
Deutschland Treffen Aussenministerin Baerbock und  U.S. Secretary of State Blinken in Berlin
Picha: Kay Nietfeld/REUTERS

Umoja wa Ulaya umetishia kuiwekea Urusi vikwazo vikubwa vya kiuchumi iwapo itaivamia Ukraine naye waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken, amekutana na marafiki wa Marekani leo kuelekea mazungumzo ya kesho atakapokutana na Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov.

Nchi za Magharibi zinataka kuonyesha msimamo wa pamoja wa kidiplomasia kabla Blinken hajakutana na Lavrov kesho mjini Geneva, katika mazungumzo yanayoonekana kama fursa ya mwisho ya kuizuia Urusi kuishambulia Ukraine kwa mara nyengine.

Katika mazungumzo na Blinken Alhamis mjini Berlin, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema Urusi itakabiliwa na vikwazo vikali mno vya kiuchumi na kifedha iwapo itafanya uvamizi huo.

Urusi itavamiwa kwa nguvu ikithubutu kuvuka mpaka wa Ukraine

Umoja wa Ulaya kupitia kwa Rais wa Halmashauri yake Kuu Ursula von der Leyen imetoa tahadhari hiyo hiyo kwa Urusi.

Deutschland Treffen Aussenministerin Baerbock und  U.S. Secretary of State Blinken in Berlin
Anthony Blinken (kushoto) akiwa na Annalean Baerbock (kulia)Picha: Kay Nietfeld/REUTERS

"Lakini hatukubali jaribio la Urusi la kuigawanya Ulaya katika nyanja za kiushawishi. Kwetu sisi, kanuni za msingi zinazosimamia usalama wa Ulaya bado ni halali katika kipengele cha mwisho cha sheria ya Helsinki na sheria ya Paris, ambazo zote zilitiwa saini na Urusi. Tunasisitiza mshikamano wetu na Ukraine na washirika wetu wa Ulaya wanaotishiwa na Urusi. Bila shaka tunaendelea kusimama na kanuni kwamba Ukraine iko huru kujiamulia mambo yake kama taifa huru," alisema Von der Leyen.

Blinken kwa upande wake amesema katika suala la Urusi kuivamia Ukraine, ushirikiano wa Marekani na marafiki zake unawapa nguvu. Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani amedai, iwapo majeshi ya Urusi yatauvuka mpaka na kuingia Ukraine basi yatakabiliwa na nguvu kali ya pamoja.

Nchi za Magharibi zinasema zinahofia Urusi inapanga shambulizi lenginedhidi ya Ukraine karibu miaka minane baada ya Urusi kuivamia Ukraine na kuliteka eneo la Crimea. Rais wa Marekani Joe Biden hapo jana alisema anaamini kwamba kuna uwezekano wa Ukraine kushambuliwa na yeye naye akasema adhabu itakuwa kali kwa Urusi.

Urusi haina mpango wowote wa kuivamia Ukraine

Lakini AlhamisUrusi ilijibu kwa kusema kitisho cha adhabu kinachotolewa na Marekani hakitosaidia kupunguza mvutano ulioko na Ukraine bali unaweza kuifanya hali kuwa mbaya zaidi.

Russlands Außenminister Sergej Lawrow
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei LavrovPicha: Dimitar Dilkoff/AFP

Urusi inasisitiza kwamba haina mpango wa kuivamia Ukraine ila wakati huo huo imetoa msururu wa matakwa - ikiwemo marufuku ya Ukraine kujiunga na Muungano wa Kujihami wa NATO - ili kuwepo na utulivu.

Marekani imeyakataa masharti hayo ya Urusi na mkuu wa NATO Jens Stoltenberg wiki hii alisisitiza kwamba muungano huo hautobadili kanuni zake za msingi kama kila taifa kuchagua mwelekeo itakaochukua.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy naye amesisitiza kwamba hakuna hakikisho la usalama wa Ulaya endapo sehemu za nchi yake zitaendelea kushikiliwa na Urusi.

Chanzo/AFP/Reuters