Blog ya kahaba wa Nairobi yaingia 10 Bora
12 Aprili 2011Baina ya tarehe 23 Februari na Machi 11, wasomaji wa blogu mbali mbali walipendekeza blogu ambayo wangelipenda ishinde tunzo ya Deutsche Welle International Blog Awards.
Mapendekezo hayo yalipitiwa na kamati maalum iliyoundwa na wataalamu wa maswala ya vyombo vya habari na waandishi maarufu wa blogu. Baadaye kamati hiyo ilichagua blogu 11 katika kila eneo zilizoingia katika duru ya pili ya uchaguzi, ambapo wasomaji wake waliipigia kura blogu wanayotaka ishinde.
Leo hii (12.04.2011) washindi wa tunzo hizo walitangazwa na ingawa Sue, kahaba kutoka Nairobi, hakuwa miongoni mwa washindi, ushiriki wake hadi kufikia kilele cha mashindano unatokana na ufanisi unaoonekana kwenye blogu yake.
"Nairobi Nights ni miongoni mwa blogu zilizoingia hatua ya mwisho ya Tunzo ya Blogu. Sababu ya kuteuliwa kwake ni kwa kuwa ina athari. Wanablogu wenye nguvu zaidi ni wale wanaotwambia hadithi zao binafsi kwa uwazi, ambazo wameziona, wamezisikia au wamekuwa ni sehemu yake, na ambazo baadhi ya wakati zinakuwa si za kuridhisha. Katika mazingira yetu, hasa kwa Kenya ambayo ni jamii ya kihafidhina, aina hii ya blogu inashtua sana." Anasema Eric Hersman, mmoja ya wajumbe wa jopo la majaji.
Kushitua huku ndiko kunakoifanya Nairobi Nights kuwa blogu ya kipekee. Ni mara ya kwanza kwa Kenya, na hata eneo zima la Afrika ya Mashariki, kwa kahaba kuyaeleza maoni yake hadharani.
Katika mikasa yake ya karibuni kabisa, Sue, ambalo si jina lake halisi, anazungumzia kukutana kwake na mwanamme mgeni kutoka Uganda na hisia zinazomwinda.
"Nimenaswa kwenye mzingiro wa fani yangu. Si kwa sababu siwezi kuiacha wakati nitakapoamua, bali ninawaza kuwa kila mtu hapa mjini anajua ninachofanya." Anaandika Sue katika mkasa aliouchapisha leo kwenye Nairobi Nights.
Jaji Eric Hersman anasema, licha ya kwamba jamii ya Kenya haikubaliani na suala la ukahaba, bado blogu ya Sue ina wafuatiliaji wengi, kwa kuwa inaeleza kile ambacho kinajuilikana lakini hakisemwi.
"Miongoni mwa mambo yanayoipa thamani blogu ni kuwafanya watu waweke makini zao kwenye vitu ambavyo wengi hawavijui au hawataki kuvifikiriana katika hali hii ni ukahaba kwenye mitaa ya Nairobi. Ndiyo unajua kuwa upo, unajua mahala ulipo, lakini hutaki kuuzungumzia."
Lau angelishinda tunzo hii, Sue angelialikwa katika sherehe ya kumkabidhi tunzo hapa makao makuu ya Deutsche Welle, Bonn, ambayo inafanyika tarehe 20 Juni, ikiwa sehemu ya mkutano wa Global Media Forum, unaowakutanisha waandishi wa habari kutoka ulimwenguni kote.
Miongoni mwa vigezo vilivyotumika kutathmini blogu za washindi ilikuwa usanifu wa lugha, uhalisia wa visa vinavyoelezwa, mtiririko wa visa na athari za yale yaliyoandikwa katika blogu kwa wasomaji, mambo ambayo kwa kiasi kikubwa yamo kwenye blogu ya Suu, Nairobi Nights.
Katika Afrika Mashariki ambako utamaduni wa kutumia blogu bado haujaenea, ushiriki wa Sue kwenye mashindano haya umethibitisha kuwa, si lazima blogu ihusu mambo mazito tu, bali mtu yeyote anaweza kuanzisha blogu na kuelezea maisha yake ya kila siku.
Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman