Blogi ya Indonesia yashinda tuzo ya blogi ya Deutsche Welle
28 Novemba 2008Blogi ni mfumo rahisi wa kuwasilisha mawazo yako kwenye mtandao wa mawasiliano wa intaneti. Hususan katika nchi ambako vyombo vya habari vinakandamizwa, blogi zimekuwa chanzo muhimu cha habari. Mwenendo huu unatakiwa kuimarishwa na tuzo ya blogi ya Deutsche Welle, kwa kifupi Bobs. Alhamisi tarehe 27 Novemba tuzo hiyo ilitolewa mjini Berlin hapa Ujerumani.
Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, idadi ya blogi imekuwa ikiongezeka kwa kasi isiyo na mithili. Kwa kutumia picha na taarifa zimeunda uliwengu wa blogi ambapo mtu anaweza kutoa maoni, kuripoti, kuwasiliana na watu wengine na taarifa zenye umuhimu mkubwa.
Si kazi rahisi kuchagua blogi iliyo bora zaidi kuliko nyengine miongoni mwa maelfu ya blogi. Kwa tuzo ya blogi ya Deutsche Welle ya mwaka huu, jopo la watu 12 wakiwemo wamiliki wa blogi na wataalamu wa vyombo vya habari wameshirikiana kutafuta blogi bora ya mwaka. Lakini kazi hiyo hawakuifanya peke yao, wamesaidiwa na watumiaji wa mtandao wa intaneti. Jamii ya watumiaji wa blogi imeshiriki sana mara hii kuliko hapo awali kuchagua blogi bora, anasema meneja wa mradi huu Gabriel Gonzales.
''Rekodi ni kwamba tumepokea mapendekezo zaidi ya 8,500 kutoka ulimwenguni kote - hili ni ongezeko la idadi hiyo kwa asilimia 20 ikilinganishwa na mwaka jana. Na pia kuna idadi nyingine nzuri ya kura 120,000 zilizopigwa wakati wa upigaji kura uliofanywa kwenye mtandao na watumiaji wetu ulimwenguni, ambao wamejitolea sana katika hili.''
Tuzo ya blogi ya Deutsche Welle inakua sambamba na ulimwengu wa blogi. Hii sio tu kupitia kushiriki kwa watumiaji. Blogi bora zimewekwa kwenye mtandao katika lugha 11.
Kwa mara ya kwanza mwaka huu blogi kutoka Indonesia zimeshiriki, nchi ambayo imeachwa nyuma katika swala la blogi. Hata hivyo wanachama wa jopo walishangwaza sana na uhalisi na mwelekeo mbalimbali wa taarifa kutoka Indonesia. Blogi ya Pitra Satvika iitwayo wazo la vyombo vya habari, ililifurahisha sana jopo hilo. Budi Putra kutoka Jakarta Indonesia ni mmoja wa wanachama wa jopo hilo
''Mwenye blogi anatueleza kuhusu kutumia blogi na jinsi ya kuandika blogi nzuri. Kwa hiyo tayari hii ni blogi maalum inayoelimisha. Napenda kupendekeza blogi hii kwa wanaomiliki blogi nchini Indonesia uwe mfano kwao na waanzishe blogi yao''
Budi Putra anafurahi pia kwamba Indonesia imeshinda tuzo ya blogi ya Deutsche Welle
''Tuzo hizi zinatambuliwa nchini Indonesia kma sehemu ya ulimwengu wa blogi. Nadhani ni vizuri kwa Indonesia, na tayari kama inavyodhihirika kw aulimwengu, Waindonesia tayari wameanzisha blogi zao.
Kutoka blogi za Ujerumani, mradi wa jumuiya ya wasichana ulichukua nafasi ya kwanza. Kaltmamsell anaeleza kwa nini blogi hii ya mambo ya wanawake ni muhimu hapa Ujerumani licha ya kuepo na uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza.
''Pia kuna mada ambazo zinapuuzwa na vyombo vya habari au ambazo zina mapungufu.Na hapo ndipo jumuiya ya wasichana inaposhughulika, kwa kuwa vuguvugu la kutaka wanawake wawe na majukumu katika jamii, ambalo lilikuwa na nguvu sana katika miaka ya nyuma nchini Ujerumani, ni nadra sana kupewa nafasi katiak vyombo vya habari vya Ujerumani. Jumuiya ya wasichana inafanya hivyo kwa njia ya blogi. Na mambo yamekuwa mazuri`''
Katrin Rönicke muandishi wa blogi ya jumuiya ya wasichana anafurahi sana kwa ushindi waliopata. Yeye pamoja na wenzake hawakuamini wameshinda kwa kuwa blogi yao imekuwepo kwa karibu mwaka mmoja tu.
'' Inasemekana hiyo ni Oscar ya ulimwenguni wa blogi. Ikiwa hiyo ni kweli, basi ina maana ni heshima kubwa kwetu na pia, kwamba katika siku za usoni tutakuwa katika ngazi ya juu ambayo tatalazimika kudhihirisha na kuonyesha kwamba tumestahili kupata tuzo hii. Hii ina maana kubblogi kila siku, kuvumbua mambo mapya na kuhakikisha zaidi usalama. Kwamba baadhi wanajaribu kuitumia vibaya, haisababishi shaka shaka kuhusu ukweli wa thibitisho hili.''
Blogi zimekuwa vyanzo muhimu vya habari katika nchi na maeneo ambako habari fulani hazizingatiwi na vyombo vya habari. Tuzo ya blogi ya Deutsche Welle inalenga kuimarisha mawasiliano kwa njia ya blogi.