Brahimi kurejea Syria kusaka suluhu
3 Oktoba 2012Taarifa za Brahimi kwenda Syria inakuwa wakati mchafuko yakiwa yamepamba moto nchini humo. Waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Riyadhi Hijab, amesema kuwa Rais Bashar al Assad alivunjika moyo wa mapatano tangu walipouawa washirika wake wa karibu mwezi Julai.
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, Jan Eliasson anasema kuwa hana uhakika kama Brahimi ataweza kutia mguu Syria lakini ana matumaini kuwa kiongozi huyo ataushawishi utawala kuelekea njia ya kupunguza machafuko.
Huenda akafanya kazi kutokea Cairo kuanza wiki ijayo na kuendelea ili awe karibu na eneo la tukio na pia aweze kushirikiana kwa ukaribu na viongozi wenziwe wa Misri.
Jan anasema " kama utawala wa Assad utapunguza mashambulizi, basi kitakachofuatia ni kupungua kwa machafuko kwa upande wa upinzani pia".
Ameongeza kuwa kuna njia mbili za kutimiza mipango ya amani na ya kwanza ni kupunguza uadui baina ya pande hizo na ya pili ni kuzionyesha kuwa mapambano ya kijeshi yanaweza kusitishwa na pande zote na kila mmoja akanufaika.
Kauli ya Muallem
Lakini hapo awali Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Walid Muallem alionyesha mashaka juu ya harakati za kutafuta suluhu nchini Syria na kusema kuwa zitafanikiwa tu ikiwa mataifa ya magharibi na yale ya kiarabu yataacha kuwaunga mkono waasi.
“Wakati serikali yangu inafanya kazi kwa juhudi kuhakikisha inawatimizia wanachi mahitaji ya muhimu watu wake waliolazimishwa na kukimbia makaazi yao na makundi yenye silaha, baadhi ya watu wanataka kuhakikisha kuwa mzozo wa wakimbizi unaongezeka kwa kuchochea makundi hayo kuwatisha raia wa Syria walioko maeneo ya mipaka na kuwalazimisha kukimbilia nchi za jirani", alisema Muallem.
Hijab: Assad hana mpango wa kupatana
Wakati Muallem akitoa shutuma hizo, aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Riyad Hijab amekiambia kituo cha televisheni cha Al-Arabiya kwamba Assad alishaweka kando matakwa ya viongozi duniani ya kupatikana suluhu nchini mwake tangu kuuawa kwa washirika wake wa karibu mwezi Julai mwaka huu.
Hijab anasema alikutana na makamu wa rais Farouq al-Shara, wabunge pamoja na viongozi wengine kwa lengo na kumshawishi Rais Assad kukubali kukaa mezani na upinzani lakini aliwajibu kuwa hataki mazungumzo na aina yoyote ya upinzani uwe wa nje au wa ndani na hawezi kufanya mazungumzo na watu waliogawanyika wasio na ajenda na wenye silaha.
Hali nchini Syria inaendelea kuwa mbaya ambapo Shirika la habari la AFP linaarifu kuwa vikosi vya serikali vimeshambulia kambi za upinzani mjini Damascus na kwamba vikosi zaidi vya kijeshi vimetumwa mjini Aleppo.
Mwandishi: Stumai George/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef