Bunge la Kenya lajadili usalama katika kivuko cha Likoni
3 Oktoba 2019Bunge la Kenya limejadili kadhia ya usalama wa shirika la Feri ambapo wabunge kutoka Mombasa wameishutumu wizara ya uchukuzi kwa kupuuza usalama wa abiria wanaotumia feri hizo. Hili linatokana na kuzama kwa mama na mwanawe baharini katika kivuko cha Likoni, mjini Mombasa, ambapo leo ni siku ya tano tangu tukio hilo litokee bado hawajaokolewa.
Wakizungumza katika bunge la kitaifa, wabunge kutoka Mombasa, wamesema wizara ya uchukuzi haikuweza kuchukua tahadhari zozote za kiusalama licha ya ilani mbalimbali kutolewa juu ya usalama wa Feri hizo. Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sharrif Nassir amesema kumekuwepo na ripoti ambazo zimekuwa zikipendekeza hatua za kiusalama kuchukuliwa lakini hilo halijafanyika.
Mbunge wa Likoni Mishi Mboko na mbunge wa Nyali Mohammed Ali wametaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya mashirika yanayohusiana na uchukuzi wa abiria baharini kando na kurekebishwa kwa miundombinu ya kivuko hicho, kuajiriwa kwa vijana walio na vipaji vya kupiga mbizi na kuwekwa kwa vituo vya dharura vya kutoa usaidizi wakati wa ajali.
Kivuko cha feri ni mojawapo wa rasilimali kuu katika sekta ya utalii na miongoni mwa pato la uchumi wa taifa la Kenya na mji wa Mombasa, ambayo pia ni njia ya kuelekea nchi jirani ya Tanzania. Kivuko hicho ndicho kinachotumiwa na kampuni mbalimbali za kubeba watalii kutoka Kazkazini mwa Pwani hadi upande wa pili wa Pwani ya Kusini kuzuru mbuga za wanyama na kukaa katika hoteli za kifahari zilizo katika fukwe za Bahari ya Hindi.
Wadau wa utalii wamekilalamikia kivuko hicho ambacho kimekuwa kikitoa taswira mbaya kutokana na kucheleweshwa kwa huduma zake. Peter Ngoko ni mfanyabiashara anayenunua mabogaboga kutoka soko kuu la Kongowea na kuzivusha bidhaa hizo hadi hoteli za kifahafari zilizoko upande wa Pwani ya Kazkazini.
Kamati ya bunge juu inayohusika na uchukuzi kwa sasa inatarajiwa kufanya uchunguzi katika shirika hilo na kuwasilisha ripoti yake bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na kutekelezwa. Shughuli za kutafuta miili hiyo leo ilichelewa kuanza kutokana na mvua inayonyesha Mombasa.
Mwandishi: Faiz Mussa