Bunge la Uingereza kupiga kura ya Brexit
15 Januari 2019Pande zote zinajiandaa kwa kivumbi cha majibizano makali, endapo mpango huo utakataliwa.
Huku kukiwa kumesalia zaidi ya miezi miwili tu hadi kufikia Machi 29 ambayo ndiyo tarehe kamili iliyowekwa kwa ajili ya Brexit, Uingereza ambayo imegawika kimtazamo pamoja na dunia inasubiri kuona kitakachotokea.
Wachache wanataraji makubaliano hayo yapite lakini jinsi Theresa May atakavyoshindwa katika kura hiyo ndilo jambo ambalo hasa litaamua iwapo atajaribu tena, ataipoteza nafasi yake kama Waziri Mkuu, atachelewesha kujiondoa kwa Uingereza kutoka kwenye Umoja wa Ulaya au hata iwapo Uingereza itaondoka kwenye umoja huo kabisa.
Makubaliano na Umoja wa Ulaya hayako kamili
Wabunge kutoka vyama vyote wanapinga makubaliano hayo kutokana na sababu tofauti lakini hapo Jumatatu May aliwataka wayatazame tena makubaliano hayo.
"Ndiyo makubaliano haya hayako kamili, lakini vitabu vya historia vitakapoandikwa watu wataangalia uamuzi wa bunge hili kesho na kuuliza, tulitimiza matakwa ya kura ya nchi yetu ya kuondoka kwenye Umoja wa Ulaya? Au tuliwavunja moyo Waingereza? Mimi nasema tuwatimizie Waingereza na kuendelea kujenga mustakabali mzuri kwa ajili ya nchi yetu," May aliwaambia wabunge.
Lakini Waziri Mkuu huyo alikuwa na hoja chache za kuongeza uungwaji mkono na wengi bado wanayapinga makubaliano hayo aliyoafikiana na Umoja wa Ulaya mwezi Novemba.
Lakini waungaji mkono sugu wa Brexit wanahofia kwamba makubaliano hayo yanaiweka Uingereza karibu sana na Umoja wa Ulaya na ni kama usaliti, huku wanaounga mkono kusalia kwenye Umoja huo wakiwa wanasema makubaliano hayo yanaifanya Uingereza iwe guu moja ndani guu moja nje.
Jeremy Corbyn anataka uchaguzi wa mapema uitishwe iwapo makubaliano yatashindwa
May aliahirisha kura kuhusu makubaliano hayo mwezi Disemba kwa kuogopa kushindwa kwa kura nyingi, lakini mambo hayajabadilika sana kutokea wakati huo. Wabunge wachache wamevuka upande wake na kumuunga mkono ila bado ni wachache sana wakilinganishwa na wanaopinga.
Kiongozi wa upinzani kutoka chama cha Labour Jeremy Corbyn amesema iwapo May atapoteza kura ya leo basi anastahili kuitisha uchaguzi wa mapema.
Iwapo makubaliano hayo yatakataliwa, basi serikali inastahili kueleza wazi kile kitakachotokea kufikia Jumatatu wiki ijayo. Kuna minong'ono kutoka pande zote kwamba huenda May akachelewesha kuondoka kwenye Umoja wa Ulaya lakini hapo jana alisema na nayanukuu maneno yake "siamini kwamba tarehe ya Machi 29 inastahili kusogezwa mbele," mwisho wa kunukuu.
Mwandishi: Jacob Safari/APE/AFPE
Mhariri: Bruce Amani