Bunge la Ujerumani laidhinisha sheria ya kurahisisha uraia
19 Januari 2024Matangazo
Serikali ya Ujerumani inasema sheria hiyo inapaswa kusaidia kuifanya Ujerumani kuwavutia zaidi wafanyakazi wenye ujuzi kimataifa na kusaidia kupunguza uhaba wa wafanyakazi.
Wabunge 382 wamepiga kura ya ndiyo na 234 hapana, huku wabunge 23 wakijizuia kupiga kura. Chini ya sheria mpya, raia wa kigeni wataweza kuomba uraia wa Ujerumani baada ya kuishi miaka mitano badala ya miaka minane.
Kwenye mazingira ambayo muombaji ametengamana vizuri na jamii, atakuwa na uwezo wa kupata uraia baada ya miaka mitatu.
Uraia wa nchi mbili kwa kawaida unaruhusiwa tu kwa raia wa nchi za Umoja wa Ulaya au Uswisi. Vyama vya upinzani vya kihafidhina ambavyo vinapinga sheria mpya vinataka mabadiliko ambayo yatalinda thamani ya uraia wa Ujerumani.