Bunge la Ulaya launga mkono mipango ya Juncker
10 Septemba 2015Wabunge wa bunge hilo la Umoja wa Ulaya pia wametowa wito wa kuitishwa kwa mkutano wa kimataifa utakaozijumuisha Umoja wa Ulaya,Umoja wa Mataifa, Marekani na Mataifa ya Kiarabu katika juhudi za kuumaliza mzozo huo mbaya wa wakimbizi kuwahi kushuhudiwa tokea kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Wabunge wamepiga kura kuunga mkono mapendekezo ya Juncker ya kugawana waomba hifadhi 160,000 walioko nchini Ugiriki,Hungary na Italia na kuwepo utaratibu wa kudumu wa kuwagawa kwa mafungu wakimbizi hao katika kukabiliana na hali za dharura kipindi cha usoni.
Azimio hilo ambalo halizibani nchi kulitekeleza kisheria limeidhinishwa kwa kura 432 dhidi ya 142 wakati wabunge 57 hawakushiriki kupiga kura.
Pendekezo la Juncker
Juncker mkuu wa halmashauri kuu ya utendaji ya Umoja wa Ulaya wenye nchi wanachama 28 amezinduwa mipango hiyo katika hotuba yake kwa bunge la Ulaya mjini Strassbourg hapo Jumatano ambapo amehimiza nchi wanachama kuyaunga mkono mapendekezo hayo kwa kusema huu si wakati wa kuhofu.
Mawaziri wa mambo ya ndani wa nchi za Umoja wa Ulaya wataitathmini mipango hiyo katika mkutano wao wa Jumatatu wakati ikikabailiwa na upinzani kutoka baadhi ya nchi wanachama za Ulaya mashariki na yumkini makao makuu ya Umoja wa Ulaya yakaitisha mkutano maalum wa kilele ili mapendekezo hayo kuweza kupitishwa.
Wabunge wanataka kufanyiwa marekebisho kwa mkataba wa Dublin wa Umoja wa Ulaya kuhusu wakimbizi ambapo kwayo maombi ya kutaka hifadhi inapaswa yasughulikiwe na nchi wanakowasili kwanza wakimbizi.
Wabunge hao wa Umoja wa Ulaya pia wamemtaka Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini kuitisha mkutano wa kimataifa kuhusu wakimbizi kwa lengo la kuanzisha sera madhubuti ya uhamiaji na kutafuta hifadhi kwa ajili ya kipindi cha usoni.
Kujumuishwa katika jamii
Wakati hayo yanajiri Kansela Angela Merkel wa Ujerumani nchi inayopokea idadi kubwa ya wahamiaji miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya Alhamisi ametembelea vituo vya kupokea wahamiaji mjini Belin na kupokewa kwa shangwe.
Wahamiaji walimpiga picha Merkel kwa kutumia simu zao za mkono wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kituo cha kushughulikia maombi ya watafuta hifadhi kituo kilioko kwenye kiunga cha Berlin.
Merkel pia ametembelea darasa la makaribisho katika shule kwa ajili ya watoto wa wakimbizi ambapo amesema kujifunza lugha ya Kijerumani na kupata ajira ni njia bora ya kuwajumuisha katika jamii maelfu ya wahamiaji wapya inaowatarajia Ujerumani.
Merkel amekaririwa akisema "Nimejulishwa binafsi leo hii juu ya kile kinachofanywa na shule nyingi mjini Berlin na nchi nzima.Inastahiki kila mtoto kumfanyia juhudi. Kuna hamasa kubwa miongoni mwa watoto na kuwa tayari kujifunza na tunataka kuwapa mustakbali mwema."
Kansela Merkel amelipongeza wazo hilo la shule za Berlin kuwa na madarasa hayo ya makaribisho ambapo watoto wa wahamiaji hujifunza sambamba na wanafunzi wa Kijerumani.
Mapema serikali yake ya mseto imewahakikishia wananchi kwamba serikali inamudu kupokea idadi isio na kifani ya watu wanaomba hifadhi nchini Ujerumani ambao wanatarajiwa kufikia 800,000 mwaka huu.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa
Mhariri :Yusuf Saumu