1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Bunge lanusuru kufungwa shughuli za serikali Marekani

21 Desemba 2024

Bunge la Marekani limepitisha muswada wa matumizi ambao umezuia kitisho cha kufungwa kwa shughuli za serikali ya kitaifa baada ya majuma kadhaa ya mivutano iliyochochewa na shinikizo kutoka kwa Rais Mteule Donald Trump.

https://p.dw.com/p/4oSJL
Bunge la Marekani
Bunge la Marekani.Picha: Liu Jie/Xinhua/picture alliance

Mabaraza yote mawili yanayounda bunge la nchi hiyo, lile la wawakilishi pamoja na Seneti yamepitisha muswada huo saa chache kabla ya muda wa mwisho wa usiku wa manane kuamkia leo ambapo shughuli za idara nyingi za serikali zingefungwa kwa kukosa fedha.

Muswada huo umeondoa moja ya kipengele kilichozusha mvutano cha kuongeza ukomo wa serikali kukopa ambacho kilikuwa kinashinikizwa na Trump ambaye ataapishwa kuiongoza Marekani mnamo Januari 20 mwakani.

Rais Joe Biden anatarajiwa kuutia saini muswada huo kuwa sheria na kuwezesha shughuli za serikali kuendelea hadi Machi mwakani. Mchakato wa kupitishwa muswada huo umeonesha mivutano ndani ya chama cha Trump cha Republican ambayo yumkini itakuwa kizingiti atakapochukua hatamu za uongozi.