1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge Zimbabwe lamuita Mugabe Mei 23

21 Mei 2018

Kamati ya bunge la zimbabwe umemuita rais wa zamani Robert Mugabe kutoa ushahidi kuhusu rushwa ya almasi inayodaiwa kugharimu mamilioni wakati wa utawala wake. Wakati huo huo Zimbabwe imeomba kurejeshwa Jumuiya ya Madola

https://p.dw.com/p/2y4X2
Robert Mugabe und Grace Mugabe
Picha: Getty Images/J.Delay

Mugabe mwenye umri wa miaka 94 na ambaye hali yake ya kiafya imedhoofika, aliitwa kutoa ushahidi mwezi uliopita lakini mkutano huo uliahirishwa. Wabunge wanapanga kumhoji kuhusiana na madai yake ya mwaka 2016 kwamba taifa hilo lilipoteza dola bilioni 15 katika mapato kutokana na rushwa na unyonyaji wa wageni katika sekta ya madini ya almasi.

Hakuna yeyote katika ofisi ya Mugabe aliyeweza kuthibitisha iwapo atahudhuria. Rais huyo wa zamani, ambaye utawala wake ulituhumiwa kujichukulia faida itokanayo na almasi, ameelezea hatua ya kumuondoa madarakani kuwa ni mapinduzi.

Zimbabwe iligundua madini ya almasi katika eneo la Chiadzwa mashariki mwa nchi mnamo miaka kumi iliopita. Makundi ya haki za binadamu yamevituhumu vikosi vya usalama kwa kutumia mbinu za kikatili kudhibiti hifadhi za madini hayo zilizotawanyika.

Kamati ya bunge inayoogozwa na mbunge wa kujitegemea temba Mliswa, tayari imewahoji mawaziri wa zamani, wakuu wa polisi na upelelezi kuhusu uchimbaji madini katika machimbo ya Chiadzwa.

Simbabwe  Emmerson Mnangagwa
Rais Emmerson Mnangagwa ameomba kuirejesha Zimbabwe katika jumuiya ya Madola.Picha: Getty Images/M.Longari

Yaomba kujiunga upya na Jumuiya ya Madola

Wakati huo huo rais Emmerson Mnangagwa ameiombea rasmi Zimbabwe kujiunga tena na jumuiya ya Madola, ilikojitoa mwkaa 2003, na ameialika jumuiya hiyo ya mataifa yaliokuwa makoloni ya Uingereza kutuma waangalizi katika uchaguzi ujao.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Patricia Scotland amesema katika taarifa kuwa Mnangagwa alituma maombi hayo Mei 15. Mnangagwa natarajiwa kutangaza tarehe ya uchaguzi mwezi huu.

"Kurejea kwa Zimbabwe katika jumuiya ya Madola kufuatia maombi ya uanachama, litakuwa tukio la kihistoria, kwa kuzingatia historia yetu ya pamoja," alisema Scotland.

Zimbabwe inatarajia kufanya uchaguzi mwezi Julai au Agosti, wa kwanza tangu Mugabe alipoondolewa, ambapo chama tawala cha Zanu-PF zinatazamiwa kushinda kwa urashi na kusalia madarakani.

Waangalizi wa uchaguzi watatoa ripoti itakayounda sehemu ya tathmini isiyo rasmi iliotumika katika maamuzi ya kuikubalia tena Zimbabwe kujiunga na Jumuwiya ya Madola," alisema Scotland.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe

Mhariri: Mohammed Khelef