Burkina Faso yawafukuza wanadiplomasia wa Ufaransa kwa uasi
18 Aprili 2024Barua ya wizara ya mambo ya nje ya Burkina Faso iliyotumwa kwa ubalozi wa Ufaransa na kuonekana na shirika la habari la AFP imewaamuru wanadiplomasia hao watatu waondoke katika taifa hilo ndani ya masaa 48.
Tangu kuingia madarakani kupitia mapinduzi ya Septemba 2022, utawala wa kijeshi umelitenga taifa hilo la Afrika Magharibi na mkoloni wake wa zamani, Ufaransa.
Soma zaidi: Watu 27 wauawa Burkina Faso
Aidha utawala huo umefuta pia makubaliano ya kijeshi ya mwaka 1961 kati ya nchi hizo mbili na balozi wa Ufaransa aliondolewa baada ya mapinduzi hayo.
Kulingana na chanzo cha Ufaransa, mnamo Disemba Mosi maafisa wanne wa Ufaransa walikamatwa na kushtakiwa mjini Ougadougou.
Mamlaka za Burkina Faso ziliwataja wanne hao kama "mawakala wa ujasusi", lakini chanzo kimoja kwenye ubalozi wa Ufaransa kilisema walikuwa ni "wahudumu wa mfumo wa teknolojia ya mawasiliano."