Burundi: Mzozo wa miaka mitatu
Mwezi Mei, tarehe 17, 2018, Waburundi wanapiga kura ya maoni ambayo huenda ikamruhusu Rais Nkurunziza kusalia mamlakani hadi mwaka 2034. Hatua ya kuongeza kipindi chake ilitokana na mzozo wa kisiasa. Ifuatayo ni ratiba.
Burundi kabla ya kura ya maoni
Tarehe 17 mwezi wa tano mwaka 2018, Warundi wanaelekea kwenye vituo vya kupigia kura kuamua iwapo Rais Pierre Nkurunziza anaweza kusalia mamlakani hadi mwaka 2034. Mazingira nchini humo ni ya wasiwasi. Mwaka 2015, maandamano yalitokea wakati Nkurunziza alipotangaza kwamba angegombea muhula wa 3. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa 1,200 walikufa katika ghasia zilizotokana na maandamano hayo.
Kipindi kingine kwa Nkurunziza?
Mwezi Aprili 2015, Rais Nkurunziza alikuwa amesalia na miezi michache ya utawala. Sheria ya Burundi inaelezea kuwa rais anastahili kuhudumu kwa kipindi cha mihula miwili, kumaanisha kuwa Nkurunziza alistahili kuachia madaraka. Hata hivyo rais huyo alitangaza kugombea kwenye uchaguzi ambao ungefuatia.
Ghasia kabla ya uchaguzi wa 2015
Maandamano katika barabara za jiji la Bujumbura yalizuka. Mwezi Mei 2015, maandamano hayo yaliongezeka na kusababisha mzozo mkubwa wa kisiasa. Mapinduzi ya kijeshi yalijaribiwa, yakazimwa. Wakati huo huo, polisi na vyombo vya usalama viliwakabili waandamanaji, huku wapinzani wa serikali wakishambulia maafisa wa usalama wa serikali. kukawepo ripoti za polisi kudhulumu na kutesa waandamanaji.
Uchaguzi tata wa urais
Tarehe 21 Julai, 2015 Warundi walielekea kwenye uchaguzi. Siku chache baadaye, Pierre Nkurunziza alitangazwa kuwa mshindi. Matokeo hayo yalitarajiwa, kwani uchaguzi huo ulisusiwa na upinzani. Mwanzoni kiongozi wa upinzani Agathon Rwasa alikataa kukubali matokeo hayo. Baadaye aliwakatisha tamaa wapinzani wengine, kwa kutaka serikali ya umoja wa kitaifa.
Wakosoaji wa serikali wanatishwa
Katika miezi iliyofuatia, vitisho vya mauaji dhidi ya wanachama wa upinzani, wakosoaji pamoja na maafisa wa serikali vilitokea kila wakati. Miongoni mwa mashambulizi makubwa ni lile dhidi ya afisa mkuu wa usalama wa Nkurunziza, Adolphe Nshimirimana na mwanaharakati Pierre-Claver Mbonimpa. Mbonimpa aliponea kifo baada ya kupigwa risasi mara nne lakini mwanaye na mkwe wake waliuawa.
Mzozo wazidi mwezi Desemba 2015
Tarehe 11 Desemba, 2015, wapinzani walishambulia kambi nne za jeshi, zilizoko Bujumbura. Siku moja baadaye, wanajeshi walivamia ngome za wapinzani katika mji mkuu. Wakaazi waliripoti vifo vingi. Takribani watu 100 walisemekana kufa wakati huo. Umoja wa Afrika ulijitolea kutuma vikosi vya kulinda amani nchini humo, lakini Nkurunziza alikataa.
Kutoroka mzozo
''Hatuwezi kupuuza mzozo wa kiwango hicho'', Adama Dieng, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa wa kuzuia mauaji ya kimbari alitangaza mwishoni mwaka mwaka 2015. Janga la kibinadamu lilikuwa limefika kileleni wakati huo. Hadi leo, wakimbizi wapatao 400,000 wa Burundi wangali wanaishi nje ya nchi hiyo.
Mazungumzo yamefeli
Januari, 2016, Umoja wa Afrika ulijaribu kuongoza mazungumzo ya upatanishi kati ya serikali na upinzani. Hata hivyo kongamano hilo lililoandaliwa mjini Arusha, Tanzania lilisusiwa mara kadhaa. Wakati mazungumzo yalianza mwezi Mei, muungano mkuu wa upinzani, CNARED, hukujumuishwa na mazungumzo hayo yalionekana kuwa yamefeli kuanzia mwanzo.
Hali ya utulivu
Kadiri siku zilivyosonga, hali ya kawaida ilirejea katika mitaa ya Bujumbura, lakini kwa kweli kulikuwa na masuala tata ya kisiasa wakati huo. Septemba, 2016, wachunguzi wa Umoja wa Mataifa walipata ushahidi wa uhalifu mkubwa wa ukiukwaji wa haki za binadamu ukiwemo mateso na mauaji yaliyofanywa na serikali. Wachunguzi pia walionya kuhusu kuongezeka kwa hofu ya kikabila.
Mageuzi ya kikatiba
Huku hayo yakijiri, serikali ya Nkurunziza ilikuwa inapanga mageuzi ya kikatiba. Mwezi Agosti, mwaka 2016, tume ya serikali ilipendekeza mabadiliko kwenye katiba ambayo yangefuta ukomo wa mihula ya urais. Nkurunziza mwenyewe aliashiria kuwa alikuwa akifikiria kuwania muhula wake wa nne madarakani hadi mwaka 2020.
Waasi wanatatiza raia
Mwanzoni mwa mwaka 2017, hali ya siasa ilisalia kuwa ya taharuki. Wanamgambo wa tawi la vijana wa chama tawala, Imbonerakure waliendelea kufanya vitendo viliyosababisha hofu miongoni mwa watu. Licha ya shinikizo za kimataifa na vikwazo kutoka kwa Umoja wa Ulaya, msimamo wa Nkurunziza haukubadilika.
Kisa cha mahakama ya ICC?
Novemba, 2017, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu iliyoko The Hague ilianzisha kesi ya madai ya uhalifu dhidi ya binadamu nchini Burundi. Mwendesha mashtaka alituhumu serikali kwa kuanzisha mashambulio ya kimakusudi dhidi ya raia. Mwezi mmoja baadaye, Burundi ikawa taifa la kwanza barani Afrika kujiondoa kutoka katika mahakama ya ICC na mkataba wa Roma.
Mauaji kabla ya kura ya maoni
Tarehe 11 Mei, 2018 wapiganaji wasiojulikana walishambulia wakaazi katika mkoa wa Cibitoke. Watu wasiopungua 26 waliuawa. Serikali ilituhumu 'magaidi' kutoka taifa jirani la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa mashambulizi hayo. Tukio hilo lilifanyika siku chache tu kabla ya kura ya maoni tarehe 17 Mei ambayo inatarajiwa kumruhu Nkurunziza kusalia madarakani hadi mwaka 2034.