Wimbi la machafuko Burundi
22 Mei 2015Tuanzie lakini Afrika kati, nchini Burundi ambako maandamano ya wapinzani wa mhula wa tatu wa rais Pierre Nkurunziza yamekuwa yakiendelea katika mji mkuu wa nchi hiyo Bujumbura licha ya kushindwa jaribio la mapinduzi na licha ya uamuzi wa rais Nkurunziza kuakhirisha hadi juni tano tarehe ya uchaguzi wa bunge na ule wa madiwani na kuwataka waandamanaji wajirekebishe.Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema Burundi imefikia ukingoni baada ya kushindwa njama ya mapinduzi.Rais Nkurunziza, linaendelea kuandika gazeti la Frankfurter Allgemeine,anahisi jukumu lake si la muda,ni la milele.Siku chache baada ya kushindwa njama ya mapinduzi,Burundi imerejea miaka 15 nyuma,katika ule wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipofikia kilele chake.Historia inajirejea,linaandika Frankfurter Allgemeine linalosema rais Nkurunziza anatumia mbinu zile zile alizopambana nazo alipokuwa kiongozi wa waasi:Ukandamizaji.Amemfukuza kazi waziri wake wa mambo ya nchi za nje kwasababu hakujua vipi kuueleza ulimwengu kuhusu azma ya rais kugombea mhula wa tatu.Muhimu zaidi amemfukuza mpaka waziri wa ulinzi,Ponitien Gaciyubwenge-jenerali anaeheshimiwa sana jeshini-na ingawa hakuna sababu zilizotolewa,lakini mwenye macho haambiwi tazama:Maandamano yalipoanza alikuwa jenerali huyo aliyepinga wanajeshi wasipelekwe kukabiliana na waandamanaji-walipelekwa baadae lakini kwaajili ya kuwalinda waandamanaji dhidi ya hujuma za polisi.
Burkina Faso si Burundi
Gazeti la mjini Berlin "die Tageszeitung "linalinganisha njama ya kutaka kung'ang'ania madaraka kuanazia nchini Burkina faso hadi Burundi.Lakini lakini wakati ambapo Burkina faso kilio cha wananchi kimepelekea rais wa zamani Blaise Compaore akitimuliwa madarakani na wanajeshi,nchini Burundi,vuguvugu la mageuzi lililoanzia katika nchi za kiarabu miaka minne iliyopita linaonyesha kugonga mwamba.Nini kitafuatia hakuna anaeweza kuashiria,linamaliza kuandika die Tageszeitung.
Mapigano yapaamba moto Sudan Kusini
Hali katika jamhuri changa ya Sudan kusini nayo pia imechambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani wiki hii.Lilikuwa gazeti la Frankfurter Allgemeine lililoandika kuhusu mapigano makali yaliyozuka huku waasi wanaoongozwa na Riek Machar wakitangaza kuvilenga visima vya mafuta katika nchi hiyo.Licha ya juhudi za mataifa jirani kuupatia ufumbuzi wa amani mzozo wa Sudan kusini,vita vinaendelea mtindo mmoja-linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeine.Mji muhimu wa mkoa wa Upper Nile-Makalal umeteketezwa.Umoja wa mataifa unahofia watu zaidi ya laki sita na nusu watajikuta katika hali ya hatari ikiwa mapigano hayatokoma.Katika mkoa jirani wa Unity hali si nyengine.Vikosi vya serikali vimeuteketeza mji wa Leer-anakotokea kiongozi wa waasi,makamo wa rais wa zamani Riek Machar.Hali inatisha kwa namna ambayo mashirika yote ikiwa ni pamoja na lile la madakitari wasiokuwa na mipaka,yameuhama mji huo.Frankfurter Allgemeine linasema katika mapigano yote hayo hakuna wanaokamatwa kama wafungwa wa vita-badala yake zimeenea ripoti kuhusu mauwaji ya raia wasiokuwa na hatia kwa hoja "wanatokea katika kabila "silo" pamoja na kulazimishwa watoto kupigana vita."
Maadini ya maeneo ya mizozo kuzuwiliwa
Lilikuwa gazeti hilo hilo mashuhuri la mjini Frankfurt-Frankfurter Allgemeine lililoandika pia kuhusu juhudi za bunge la Umoja wa Ulaya kutaka kuanzisha sheria inayoyapiga marufuku makampuni ya nchi wanachama kununua maadini kutoka nchi zinazokumbwa na vita vya wenyewe ili kukomesha mtindo wa kugharamiwa mizozo kwa fedha za maadini hayo.Wengi wa wabunge wameunga mkono pendekezo la halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya kuhusu marufuku hayo.Makampuni ya nchi za Umoja wa Ulaya yanabidi hivi sasa kuonyesha hati zinazobainisha bishara ya maadini imefanyika kwa njia ya uwazi.Baada ya bunge la Ulaya mjini Brussels,itakuwa zamu hivi sasa ya baraza la mawaziri kuzungumzia suala hilo.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/PRESSER/ALL/Presse
Mhariri: Mohammed Khelef