Burundi yatangaza siku 7 za kumuomboleza Rais Nkurunziza
10 Juni 2020Matangazo
Tangazo la serikali kwenye Redio na Televisheni ya taifa lililosomwa na msemaji wake Prosper Ntahorwamiye ambaye pia ni Katibu mkuu wa serikali lilisema Nkurunziza alifariki dunia kutokana na mshituko wa moyo katika hospitali ya mkoani Karuzi.
Kulingana na katiba ya Burundi spika wa Bunge Pascal Nyabenda ndiye atakayeshika hatamu za uongozi kwa kipindi cha miezi miwili hadi atakapotawazwa Evariste Ndayishimiye aliyeibuka na ushindi kwenye uchaguzi wa rais wa Mei 20 mwaka huu.
Hata hivyo taarifa nyingine zinasema muhula wa bunge ulimalizika tangu April 27 ilipozinduliwa kampeni ya uchaguzi hivyo ni makamu wa rais atakayeshika hatamu.
Nkurunziza aliiongoza Burundi kwa kipindi cha miaka 15.