Burundi yatoa waranti wa kumkamata Buyoya
1 Desemba 2018Mwendesha mashitaka mkuu wa Burundi Sylvestre Nyandwi amesema uchunguzi umebainisha kuwa watu hao walihusika katika kupanga na kutekeleza mauaji dhidi ya Ndadaye, rais wa kwanza wa nchi hiyo aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, wa kwanza pia kutoka jamii ya Wahutu. Mauaji hayo yalifuatiwa na machafuko makubwa ya kikabila, ambamo watu zaidi ya 300,000 waliuawa.
Buyoya kwa wakati huu ni mwakilishi wa Umoja wa Afrika nchini Mali, na ni mtu anayeheshimiwa barani Afrika na katika jumuiya ya kimataifa. Buyoya, Mtutsi aliyeingia madarakani kupituia mapinduzi ya kijeshi mwaka 1987 alikubali kushindwa na Ndadaye katika uchaguzi wa mwaka 1993.
Lakini Ndadaye alihudumu madarakani kwa miezi minne tu, akauawa na kundi la wanajeshi Watutsi wenye misimamo mikali, katika jaribio la mapinduzi lililoitumbukiza Burundi katika mzozo ambao athari zake zinaendelea hadi leo.
Katika waranti wake, Burundi inazitaka nchi wanakoishi washutumiwa hao kuwakamata na kuwarejesha nchini kwao, ikisema ni muhimu watu hao kuhojiwa kuhusu mchango wao katika mauaji ya Ndadaye.
Miongoni mwa 16 wanaotuhumiwa pamoja na Buyoya, 11 walikuwa maafisa wa kijeshi, na 5 waliobakia walikuwa raia wenye mahusiano ya karibu na Buyoya.
Serikali ya sasa ya Burundi inaongozwa na chama cha Cndd-FDD cha Rais Pierre Nkurunziza, kikiwa tawi la kundi la zamani la waasi wa kihutu.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe
Mhariri: Iddi Ssessanga