Wanadiplomasia wa mataifa makubwa wakutana kuijadili Haiti
11 Machi 2024Mkutano huo unafanyika wakati machafuko ya magenge ya uhalifu yakisambaa katika mji mkuu wa taifa hilo maskini kabisa la kisiwa cha Karibiani na kuwalazimisha wanadiplomasia wa kigeni kukimbia mwishoni mwa wiki.
Makundi ya uhalifu, ambayo yanadhibiti sehemu kubwa ya Port-au-Prince pamoja na barabara zinazoelekea maeneo mengine ya nchi, yamesababisha vurugu katika siku za karibuni, huku yakijaribu kumuondoa madarakani Waziri Mkuu Ariel Henry.
Soma zaidi: Mji mkuu wa Haiti wakabiliwa na hali mbaya kutokana na machafuko
Muungano wa mataifa ya Karibiani (CARICOM) umewaalika mabalozi kutoka Marekani, Ufaransa, Canada, na Umoja wa Mataifa katika mkutano wa kujadili machafuko hayo na njia za kutoa msaada kwa Haiti.
Marekani iliwaondoa kwa kutumia ndege wafanyakazi wake ambao majukumu yao si ya lazima kwenye ubalozi wake mjini Port-au-Prince.
Aidha jeshi la Marekani lilifanya operesheni ya kuimarisha ulinzi wa ubalozi wake ili kuwezesha shughuli za ubalozi kuendelea.
Balozi wa Ujerumani alihamia Jamhuri ya Dominican pamoja na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya.