CCM, na CUF zaendelea na kampeni za urais Tanzania
29 Septemba 2020Msafara wake umeonekana kusimama mara kadhaa njiani akiwasalimia wananchi, kuwaombea wabunge na madiwani wa chama chake katika maeneo husika ikiwemo maeneo ya mbalali na kuwaelezea tayari amelifanyia nini taifa tangu alipoingia mamlakani mwaka 2015.
Katika viwanja vya makambako mkoani Njombe rais Magufuli akisindikizwa na wananchama wakongwe wa chama chake akiwemo makamu mwenyekiti wa CCM Philip Mangula, ameonekana kutumia muda mwingi katika kuelezea namna ambavyo ataendelea kutatua changamoto za wanachi katika eneo hilo ambalo linatajwa kuwa na wakulima wakubwa wa kilimo cha chai pamoja na maparachichi.
Amesema endapo atachaguliwa tena atahakikisha maendeleo ya watu yanafikiwa kutokana na serikali kutengeneza mazingira wezeshi kwa wananchi katika sekta mbalimbali kwa kuzingatia kuendeleza miradi ya kimaendeleo ikiwemo maji, nishati pamoja na kuwaunganisha na dunia kwa kuboresha kiwanja cha ndege kitakachobeba mazao kupeleka nje ya nchi kwa ajili ya soko.
Katika kusisitiza wapiga kura wanashiriki zoezi la uchaguzi kwa amani na utulivu, makamu mwenyekiti wa chama cha mapinduzi Phiilip Mangula, amewaambia wapiga kura wanatakiwa kumaliza kupiga kura na kurejea nyumbani na kusubiri majibu, na si kulinda kura sababu wakala wapo kwa ajili ya kuwawakilisha.
Wakati mgombea wa CCM akiendelea na kampeni zake huko nyanda za juu kusini, mgombea wa kiti cha urais kupitia chama cha wananchi CUF Profesa Ibrahim Lipumba, amezungumza na wananchi wa mkoa wa shinyanga katika jimbo la ushetu ambappo mbali na mambo mengine amesisitiza rais atakayechaguliwa lazima ajue changamoto za wananchi, hivyo kuwahimiza mabadiliko.
Siku ya Jumatano mgombea wa chama cha mapinduzi Rais John Magufuli anatarajiwa kuzungumza na wapigakura wa mkoani Mbeya eneo ambalo siasa zake zinaangaliwa kuwa na ushindani mkubwa, kutokana na eneo hilo kuongozwa na upinzani kwa miaka 10.
Na Hawa Bihoga Dw Dar es salaam