1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CDU kumpitisha tena Merkel

9 Desemba 2014

Wana Christian Democratic wa Ujerumani wanatarajiwa kumchagua kwa sauti moja kansela anaependwa na umma, Angela Merkel kuendelea kuwa mwenyekiti wao wakati wa mkutano wao mkuu unaoanza katika jiji la Cologne.

https://p.dw.com/p/1E1LH
Mkutano mkuu wa CDU wafunguliwa ColognePicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Mkutano huo wa siku mbili unaohudhuriwa na zaidi ya wajumbe elfu moja katika mji huo wa magharibi ya Ujerumani unafanyika katika wakati ambapo Angela Merkel anaiongoza kwa karibu mwongo mmoja nchi muhimu zaidi kiuchumi barani Ulaya na kuendelea kujivunia umashuhuri kumpita kiongozi yeyote yule mwengine ulimwenguni.

Uchunguzi wa maoni ya umma uliosimamiwa hivi karibuni na kituo cha kwanza cha televisheni cha Ujerumani ARD umeonyesha asili mia 67 ya wajerumani wanamuunga mkono Angela Merkel.Asili mia 56 wanamtaka aendelee na mhula wa nne kama kansela madarakani kuanzia mwaka 2017 na takriban robo tatu ya wajerumani wanataraji atagombea tena wadhifa huo uchaguzi mkuu utakapoitishwa-hayo ni kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliochapishwa jumapili iliyopita na gazeti la Bild.

Katika wakati ambapo wakaazi wengi wa nchi za kusini mwa Ulaya wanasumbuliwa na shida za kiuchumi na migogoro ya fedha katika kanda ya Euro kutokana na shinikizo la Merkel la mageuzi na hatua za kufunga mkaja,wajerumani wengi wanamwangalia kama baraka iliyoiokoa nchi hii katika bahari ya misuko suko.

Angela Merkel,binti ya kasisi wa kiluteri ,mwanafizikia mwenye umri wa miaka 60 aliyekulia Ujerumani mashariki ya zamani ,anakiongoza chama cha Christian Democratic CDU tangu mwaka 2000 na amekuwa akichaguliwa kuwa kansela tangu mwaka 2005.Na hakuna dalili nani atamrithi baadae.

Ni aina mpya ya uongozi anasema Wolfgang Schäuble

Waziri wa fedha Wolfgang Schäuble alimsifu bibi Merkel wiki hii na kuulinganisha mtindo wa uongozi wake na ule wa Ufaransa katika karne ya 19 chini ya kiongozi wake wa kisiasa na kijeshi Napoleon.Waziri huyo mkongwe ameliambia gazeti la Süddeutsche" Merkel amefanikiwa vyema zaidi kuliko viongozi wote wengine wa Umoja wa ulaya kuwakilisha jamii ya mchangayiko wa watu tofauti."Hii ni aina mpya ya uongozi-ni bora zaidi kuliko ule wa Napolreon amesema.

Merkel beim CDU Parteitag in Köln 09.12.2014
Kansela Angela Merkel akihutubia wajumbe mkutanoniPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Mikutano mikuu ya chama cha CDU imegeuka uwanja wa kusherehekea ufanisi wa kansela aliyepewa jina la Muttti au Mummy na hata kuitwa Angie na wafuasi wa chama kinachoitwa kwa dhihaka "kilabu ya kumchagua kansela".

Katika mkutano wa CDU ulioitishwa miaka miwili iliyopita,Angela Merkel alijikingia asili mia 97.9 ya kura.Alikuwa kansela wa kwanza wa Ujerumani Konrad Adenauer,mwasisi wa chama hicho cha CDU aliyewahi kujikingia asili mia mia moja ya kura katika mikutano mikuu mitatu mfululizo ya chama hicho katika miaka ya "neema ya kiuchumi 1954,56 na 1958.

Umoja na mshikamano nyuma ya Merkel

Hakuna mabadiliko makubwa yanayotarajiwa kutokea katika mkutano mkuu huu utakaomalizika kesho mjini Cologne.

Volker Kauder PK zum Irak Besuch 26.08.2014 Berlin
Mkuu wa kundi la CDU bungeni Volker KauderPicha: picture-alliance/dpa

Katika wakati ambapo walimwengu wanakodolea macho mzozo wa Ukraine na Syria,Ebola na mabadiliko ya tabia nchi,mada kuu zinazoweza kuzusha mabishano katika mkutano mkuu wa CDU zinatarajiwa kuhusiana na masuala ya ndani ikiwa ni pamoja na nyongeza za mishahara na malipo ya juu ya kodi za mapato.

Mkuu wa kundi la CDU katika bunge la shirikisho,Volker Kauder amewataka wajumbe mkutanoni wawe na msimamo mmoja.Ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa tunanukuu:"Tunabidi kudhihirisha mambo mawili;kwanza tuko nyuma ya Angela Merkel na mkondo wake na pili tunapigania ubunifu na ukuaji wa kiuchumi."Mwisho wa kumnukuu.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu