1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CHADEMA yaja na mkakati wa kuimeza CUF Zanzibar

Hawa Bihoga11 Septemba 2018

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA kimesema kitawashawishi wabunge wa chama cha wanachi CUF kwa upande wa Zanzibar, ili kuchukua kadi za chama hicho kwa malengo ya kukiondoa chama tawala CCM ambacho kimeongoza taifa hilo kwa zaidi ya miongo mitano sasa.

https://p.dw.com/p/34gkL

Baraza la wazee la Chadema limesema hata kiongozi wa chama cha CUF Maalim Seif Sharif Hamad watamshawishi ajiunge na chama hicho ili agombee nafasi ya urais kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2020, huku wabunge wa CUF wakisema ni mapema mno kufikia maamuzi ya kujiunga na CHADEMA. 

Hashim Juma Issa, mwenyekiti wa baraza la wazee wa chama cha demokrasia na maendeleo chadema, mbele ya waandishi wa habari ameeleza sababu kuu za baraza hilo kufikia maamuzi ya ushawishi kwa wabunge wa chama cha CUF kujiunga na chama hicho kwa malengo ya kukitoa mamlakani chama tawala CCM kwa upande wa Zanzibar.

Tansania Daressalam | Chadema Ältestenrat
Mwenyekiti wa baraza la wazee wa Chadema Hashim Juma Issa akihutubia mkutano wa waandishi habari jijini Dar es Salaam, Septemba 11, 09.2018.Picha: DW/S. Khamis

Mbali na chama cha CHADEMA pamoja na CUF kuwa katika muungano wa vyama vya upinzani nchini humo unaotambulika kama UKAWA, na itakumbukwa kwamba katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2015 muungano huo wa vyama vya siasa ulimsimamisha mgombea wa nafasi ya urais waziri mkuuu mstaafu Edward lowasa katika kuwania nafasi ya urais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Nguvu hii ya umoja pamoja na ushawishi mkubwa wa Maalim Seif kwa wazanzibari vinatajwa na mwenyekiti wa baraza hilo la wazee kutoka chama hicho pinzani kuwa, huenda itasaidia katika mipango ya kuiondosha CCM mamlakani katika visiwa hivyo, ambapo ameiambia dw tayari yeye binafsi ameshaanza mazungumzo na maalim seif na matumaini anaona yanaridhisha.

Katika hili baadhi ya wabunge wa CUF waliozungumza na dw wanasema kuwa, ni mapema kufikiria na kuamua maamuzi ya kukihama chama hicho ambacho kimekumbwa na mgogoro wa kiongozi uliosababisha kukigawa chama na kuongeza kuwa hadi kufikia elfu mbili na ishirini chama kitarudi kuwa taasisi imara kama hapo awali.

Duru za kisiasa nchini humo zinabainisha kuwa,hili lilitegemewa kutokea kutokana na tayari chama cha CUF kipo katika mgogoro wa kiuongozi, na kukitaka chama hicho kufanya maamuzi ambayo yataleta tija kwa wananchama na wafuasi wa chama hicho cha upinzania chenye nguvu zaidi visiwani Zanzibar.

Mwandishi: Hawa Bihoga Dw Dar es salaam
Mhariri:Josephat Charo