Chama cha RN chaongoza duru ya kwanza uchaguzi wa Ufaransa
1 Julai 2024Chama cha mrengo wa kulia nchini Ufaransa cha National Rally RN, kimepata mafanikio ya kihistoria yaliyokiwezesha kushinda duru ya kwanza ya uchaguzi wa bunge uliofanyika siku ya Jumapili, kulingana na matokeo ya awali.
Chama hicho kinachoongozwa na mwanasiasa Marine Le Pen, kinatazamiwa kupata asilimia 34 ya kura, kikiwa mbele ya vyama vya mrengo wa kushoto na vile vya wastani ikiwemo chama cha Rais Emmanuel Macron cha Muungano wa pamoja kinachotajwa kupata asilimia kati ya 20 hadi 23.
Ikiwa hakuna mgombea atafikisha asilimia 50 ya kura katika duru ya kwanza, wagombea wawili wa juu watafuzu moja kwa moja kuchuana duru ya pili, itakayofanyika Julai 7.
Rais Macron aliitisha uchaguzi wa mapema baada ya chama chake kuangushwa na chama cha siasa kali katika uchaguzi wa bunge la Ulaya uliomalizika mapema mwezi uliopita.