Chama mshirika wa Merkel jimbo la Bavaria mashakani
14 Oktoba 2018Chama cha Christian Social Union , CSU, ambacho kimekuwa kikilitawala jimbo hilo bila msaada wa chama kingine tangu mwishoni mwa miaka ya 1950, kinatarajia kupoteza wingi wake katika bunge la jimbo hilo, kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni.
Washirika wengine katika muungano tete wa serikali unaoongozwa na Merkel , unaojulikana kama "muungano mkuu" chama cha Social Democratic, SPD, pia wanatarajiwa kupoteza viti vingi wakati chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kinachopinga wahamiaji cha AfD kinaonekana kupata uhakika wa kuingia katika bunge la jimbo hilo.
Washindi wakubwa katika uchaguzi huo , hata hivyo, huenda wakawa chama cha mrengo wa kushoto cha walinzi wa mazingira , Greens ambao wameongeza maraduru mvuto wao kwa wapiga kura hadi asilimia 19 tangu uchaguzi wa mwisho uliopita katika jimbo hilo, hali inayoweza kukifanya chama hicho kuwa chama cha pili chenye nguvu katika jimbo hilo.
Watu milioni 9.5 wenye haki ya kupiga kura walitarajiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura vilivyofunguliwa asubuhi saa 12 kwa saa za Ulaya ya kati. Iwapo uchunguzi wa maoni ya wapiga kura utakuwa sahihi, uchaguzi wa jimbo la Bavaria utaonesha hatua nyingine katika kuporomoka kwa mwanvuli wa vyama vikubwa na kuvunjika kwa uwanda wa kisiasa , kama inavyoonekana katika mataifa mengine ya magharibi.
Kiongozi dhaifu
Kwa Merkel , ambaye kwa sasa mara kwa mara huonekana kama kiongozi asiye na nguvu tena katika muhula wake wa nne madarakani na wa mwisho, itasababisha hali ya wasi wasi zaidi wa kisiasa wiki mbili kabla ya uchaguzi mwingine hata, katika jimbo la kati la Hesse.
Spika wa bunge la Ujerumani Wolfgang Schaueble , mshirika wa muda mrefu wa Merkel , amekiri kwamba uchaguzi katika majimbo hayo mawili , utakuwa na athari katika siasa za taifa na kuathiri pia heshima ya kansela," ambaye anawania kuchaguzi tena kama mkuu wa chama cha Christian Democratic Union , CDU mwezi Desemba.
Chama ndugu cha CSU cha jimbo la Bavaria kwa chama cha Merkel cha CDU, kimekuwa kwa muda mrefu kikikumbatia aina ya siasa za kilabu ya pombe na kudhibiti madaraka katika jimbo hilo linalofahamika sana kwa kuwa na makasri, sherehe za kunywa bia zinazofahamika kam Oktoberfest, kamapuni makubwa kama Siemens na BMW pamoja na klabu kubwa tajiri ya kandanda ya Bayern Munich.
Chama hicho kimekuwa kikinadi uthabiti wa kiuchumi pamoja na maadili ya kihafidhina katika jimbo hilo amablo wakaazi wake wengi ni Wakatoliki, wakihimiza kuwapo misalaba katika madarasa ya shule na kupiga marufuku uvaaji wa hijabu hadharani kwa Waislamu.
Kama chama ambacho kilikuwa wakati wote kikipata kura nyingi, chama hicho kutoka katika kile kinachoitwa jimbo huru la Bavaria kimekuwa kikitawala kwa pamoja na chama cha Merkel cha CDU mjini Berlin katika serikali kuu.
Lakini hali hiyo ilibadilika baada ya katikati ya mwaka 2015, wakati jimbo hilo linalopakana na Austria ghafla likawa jimbo la msitari wa mbele nchini Ujerumani kwa mmiminiko wa wakimbizi wengi wao wakiwa Waislamu na mahamiaji wengine, nusu yao kutoka Syria , Iraq na Afghanistan.
Baada ya hali ya awali ya kuwakaribisha , mmiminiko huo ulizusha mapambano ya chuki dhidi ya wageni ambayo yalisababisha taifa hilo kujitokeza kwa chama cha AfD, ambacho katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana kilichukua mamilioni ya wapiga kura na kudhoofisha vyama vyote vikubwa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Yusra Buwayhid
Mhariri: Yusra Buwayhid