Chama tawala Taiwan chashinda uchaguzi wa rais
13 Januari 2024Mgombea wa chama tawala katika kisiwa cha Taiwan cha Democratic Progressive DPP, Lai Ching-te ameshinda katika uchaguzi wa rais. Chama cha Lai kinachopambania Taiwan kuwa na utambulisho wake na kukataa madai ya China kuwa kisiwa hicho ni sehemu yake, kilikuwa kikitafuta muhula wa tatu.
Soma pia: Kura zaanza kuhesabiwa katika uchaguzi muhimu wa Taiwan
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Lai amesema kuwa watu wa Taiwan wamefanikiwa kuzishinda juhudi kutoka nje ya kisiwa hicho zilizokuwa na lengo la kuingilia uchaguzi. Ameapa kuilinda Taiwan dhidi ya vitisho vya China.
Mgombea wa chama kikuu cha upinzani cha KMT, Hou Yu-ih amekubali kushindwa na kuwaomba msamaha wafuasi wake kwa kushindwa kukiondoa chama tawala madarakani katika uchaguzi ambao China iliutaja kuwa unamaanisha kuchagua kati ya vita na amani.
Kando ya Hou, Lai alikuwa akikabiliwa pia na upinzani kutoka kwa mgombea Ko Wen-je wa chama kidogo cha Taiwan People's Party ambaye aliwahi kuwa Meya wa Taipei. Umoja wa Ulaya umewapongeza wapiga kura wa Taiwan kwa kushiriki katika zoezi hilo la kidemokrasia.