1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama tawala Uturuki chaponea chupuchupu kupigwa marufuku

Kalyango Siraj31 Julai 2008

Kinalaumiwa kutaka kuanzisha utawala wa sheria za dini

https://p.dw.com/p/Ennz
Wafuasi wa waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan wakipeperusha bendera za Umoja wa Ulaya pamoja na za taifa laoPicha: AP

Chama tawala nchini Uturuki cha AKP kimeponea chupuchupu kupigwa marufuku kutokana na madai kuwa kilikuwa kinajaribu kuvuruga mfumo wa taifa hilo wa kutoiingiza dini katika masuala ya serikali.

Majaji sita kati ya wote 11walipiga kura ya kukipiga marufuku lakini kasoro ya kura moja tu inayohitajika ya watu saba.Hata hivyo mahakama hiyo imekubali kukionya chama cha waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan kwa kuwa mwaka huu ni lazima kipate nusu ya msaada kutoka kwa serikali.

Mahakama ya kikatiba ya Uturuki imemaliza hali ngumu ya kisiasa iliolikumba taifa hilo kwa miezi kadhaa. Majaji sita kati ya wote 11 walipiga kura ya kukipiga marufuku chama hicho.Hali ikiwa ya wasiwasi matokeo yakatangazwa.

Matokeo hayo yalionesha kuwa hoja ya kukipiga marufuku chama tawala cha AKP imeshindwa kwani,ili kuweza kupita kura zingekuwa saba na wala sio sita.

Mwendesha mashataka mkuu aliwasilisha kesi hiyo mwezi machi akidai kuwa siasa za jamhuri ya Uturuki ziko hatarini kuliko ilivyokuwa kabla.

Alitaka chama cha AKP kupigwa marufuku pamoja na na wajumbe wake kadhaa wa chama hicho akiwemo waziri mkuu,kutojihusisha katika siasa.

Lakini chama cha AKP daima kimekuwa kinakanusha madai hayo, na viongozi wake ambao wakati mmoja walikuwa wanachama wa vyama vinavyoegemea dini ya kiislamu,wanasema kuwa sasa wamebadilika.

Uamuzi wa majaji wa kutokipiga marufuku chama hicho unaonekana kama dawa muafaka kuelekea wasiwasi wa kisiasa ambao umekuwa umetanda nchini humo.

Waziri wa Uturuki wa masuala ya Utamaduni ambae ni kutoka kwa chama tawala cha AKP Ertugrul Guyan alisifu matokeo hayo.

Ingawa wananchi walipumua lakini mahakama hiyo imetilia mkazo kuwa inatoa ujumbe mkali kwa chama hicho kwa kuamuru kuwa kipewe nusu ya mgawo wake kutoka kwa serikali mwaka huu kama onyo.

Na majaji waliounga mkono uamuzi wa kukipunguzia mgawo wake walikubali kuwa chama hicho kimekuwa kama kiini cha shughuli zinazopinga utawala usioegemea dini, ingawa kama alivyosema jaji kuwa hali haikuwa mbaya zaidi kuweza kukipiga marufuku chama hicho.

Waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan alifurahia matokeo hayo akisema kuwa yataimarisha demokrasia ya Uturuki na kuahidi kulinda utawala usiopendelea kuingiza dini katika masuala ya kisiasa.

Chama cha AKP ambacho kilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwaka jana kimekuwa kinalaumiwa kutaka kuanzisha utawala unaoegemea sheria za dini yaa kiislamu.Hata hivyo chama hicho kimepinga kabisa madai hayo.