Chelsea yaingia fainali ya Ligi ya Mabingwa
25 Aprili 2012Chelsea ilifuzu kwa jumla ya magoli 3 kwa 2, baada ya kushinda goli moja kwa sifuri ktika mkondo wa kwanza tarehe 18 mwezi huu wa Aprili mjini London.
Kiungo Mbrazil Ramires na mchezaji alieningia kama nguvu mpya Frenando Torres waliifungia Chelsea magoli hayo muhimu ya ugenini, baada ya Sergio Busquests na Andres Iniesta kuipa Barca uongozi wa magoli mawili kwa bila. Chelsea walilazimika kucheza kipindi kirefu cha mchezo bila ya huduma za nahodha wao John Terry, aliyetimuliwa uwanjani kwa kumchezea vibaya Alexis Sanchez. Mchezaji bora wa ulimwenguni wa FIFA Lionel Messi alipoteza penalty kwa upande wa Barca. Torres aliingia zikiwa zimesalia dakika kumi kumpumzisha Drogba, na akafunga bao lake katika dakika ya mwisho ya muda wa majeruhi.
Kulipiza kisasi
Matokeo hayo yalikuwa kulipiza kisasi kwa Chelsea, ambayo ilizuiwa na Barcelona kuingia katika fainali kwa njia ya utata mnamo mwaka wa 2009 kutokana na sheria ya bao la ugenini.
Katika fainali ya mwaka huu itakayochezwa tarehe 19 mwezi Mei mjini Munich, Chelsea watakutana na Bayern Munich au Real Madrid, ambao watamaliza mchuano wao wa nusu fainali leo Jumatano nchini Uhispania.
Bayern walishinda mkondo wa kwanza magoli mawili kwa moja. Chelsea hawajawahi kushinda Ligi ya Mabingwa. Walishindwa na Manchester United katika fainali ya mwaka wa 2008 kupitia mikwaju ya penalty mjini Moscow.
Mkufunzi wao wa muda Roberto Di Matteo hata hivyo hakukubali kuwa huo ulikuwa mchezo wa kulipiza kisasi kutokana na kichapo chao mwaka wa 2009. alisema hawakutaka kulipiza kisasi, bali kucheza mchezo wao.
Kwamba miaka mitatu iliyopita, mambo yalikuwa mazuri kwa Barcelona lakini wakati huu yameenda vyema kwetu. Labda ilikuwa hatima.
Terry aomba radhi
Naye nahodha wa Chelsea John Terry ameomba msamaha kutokana na kadi yake nyekundu aliyopewa, ambayo itamweka nje ya fainali ya kombe hilo. Terry alisema yeye siyo aina ya mchezaji anayemuumiza yeyote kimakusudi.
Di Matteo alichukua wadhifa huo kutoka kwa Andres Villas Boas mwezi Machi na huenda akapewa kazi hiyo kwa mkataba wa kudumu baada ya kuwaongoza the Blues hadi fainali ya Ligi ya Mabingwa na kombe la FA.
Wakati huo huo, beki wa Barcelona Gerard Pique alikesha hospitalini baada ya kuanguka na kuzirai wakati wa mchuano huo. Pique aliondoka uwanjani katika dakika ya 25, dakika tisa baada ya kugongana na mwenzake mlinda lango Victor Valdes wakati walipoung'ang'ania mpira uliokuw aukikimbiliwa na Didier Drogba. Pique alisalia chini kwa muda bila kujifahamu kabla ya kunyanyuka.
Rais wa Barcelona Sandro Rosell alikitaja kichapo hicho kuwa ni “pigo kuba kwao” lakini akaipongeza Chelsea. Alisema anajivunia mashabiki wao ambao wamekuwa na wiki ngumu lakini wakaonyesha ukomavu. Barca ilishindwa na Real Madrid jumamosi magoli mawili kwa moja. Barca iliumiliki mpira kwa asilimia 75 wakati Chelsea wakilikinga lao lao.
Mwandishi: Bruce Amani/dpa/Reuters
Mhariri: Oumilkheir Hamidou