China: Baada ya Google, sasa kuipiga marufuku Skpe?
4 Januari 2011Ikiwa na takribani watumiaji milioni nne na nusu wa huduma ya mtandao, China ndilo taifa lenye idadi kubwa zaidi ya watumiaji wa huduma hii ya mawasiliano ya kisasa, lakini ni miongoni mwa nchi zenye kiwango cha chini cha uhuru wa mtu binafsi.
Hivi sasa serikali ya nchi hiyo inataka kuifungia huduma ya kupiga simu kwa kutumia mtandao wa kompyuta, kwa kile kinachoitwa na Wizara ya Habari ya nchi hiyo, hatua ya kupambana na matumizi yasiyo halali ya huduma za simu.
Hapana shaka, machungu ya kufungiwa kwa huduma ya kampuni kama vile Sykpe ambazo hutoa huduma ya simu bure au kwa bei nafuu sana, kutawaathiri watumiaji kama Zhang Yufan, ambaye amekuwa mtumiaji wa Skpe kwa miaka sasa.
"Watu wanaofanya kazi nje ya nchi huwa wanapiga simu huku nyumbani kwa kutumia mtandao. Na familia ambazo zina watoto wao wanaosoma nje wanatumia huduma hii pia. Mimi nilianza kutumia huduma hii pia, kwa sababu nilikuwa na jamaa wanaoishi mbali. Kila siku nilikuwa natumia masaa mawili kupiga simu kwenye mtandao. Wakiizuia Skpe, itanilazimu kutumia ujuzi wangu wa kompyuta kugundua njia nyengine. Labda msambazaji wa huduma hii nje ya nchi ili niweze kutumia Skpe. Na hilo likishindikana, itabidi ninyanyue mikono." Anasema Zhang.
Kiasi ya watu milioni 10 na 20 hutumia huduma hii kwa kompyuta, na kwa hivyo wakaweza kunusuru pesa nyingi zinazokwenda kwenye mawasiliano. Kwa mfano, wakati mazungumzo ya simu ya kawaida kutoka kutoka China kwenda Marekani hugharimu senti 80 za sarafu ya Euro, sawa na dola moja ya Kimarekani, kwa Skpe inagharimu senti mbili tu. Hii maana yake ni kuwa makampuni makubwa ya simu nchini China, yanakosa asilimia 70 ya pato ambalo ingelilipata ikiwa watumiaji wote wa simu wangelitumia huduma yao, badala ya mtandao, ambayo sasa huenda kwa makampuni ya Skype, Google, MSN na vikampuni vyengine vidogo vidogo vinavyotoa huduma hii nchini China.
Kan Kaili wa Chuo Kikuu cha Posta na Simu anasema hili la kuyazuwia makampuni hayo kutoa huduma ya simu za mtandao huedna likawa limechochewa na wakubwa wa serikali na jeshi la polisi.
Gazeti la Hong Kong ambalo linapingana na mpango huu, South China Morning Post, linasema kwamba baada ya machafuko ya umwagaji damu kwenye jimbo la Xinjiang mwezi Julai 2009, makampuni ya simu yalipata amri kutoka kwa mamlaka ya serikali kurekebisha huduma zao za simu zinazotumia mtandao, maana walikuwa wamepata ushahidi wa kimazingira unaoonesha kuwa wapinzani wa serikali wanatumia mtandao kupanga mambo yao.
Lakini Kaili anaona kuna sababu za ziada, zikiwemo za ukiritimba wa makampuni makubwa ya simu nchini China, ambayo yanamilikiwa na serikali.
"Matumizi ya simu kupitia mtandao yanakuwa kwenye mikono ya mtu binafsi. Hili linaifanya biashara kwa makampuni matatu makubwa ya simu ya serikali kuwa ngumu. Kwa hivyo, uwezekano kwa serikali kuonesha inavyokerwa na jambo hili. Na nani ambaye serikali inamuhofia hapa? Watumiaji au makampuni. Ni wazi kuwa, maslahi ya serikali ndiyo yanayoangaliwa hapa." Anasema Kaili.
Hata hivyo, kwa mujibu wa wataalamu wa mawasiliano, uwezekano wa kuyadhibiti mawasiliano ya simu kupitia mtandao, ni mdogo. Kwa hivyo, itabidi China itekeleze ule msemo tuchekeane tusiumizane, ili kila mmoja, baina ya makampuni makubwa ya serikali ya simu, makampuni ya mitandao na watumiaji wa huduma hizi, awe salama.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Astrid Freyeisen/ZPR
Mhariri: Othman Miraji