China kutohudhuria mkutano wa "Marafiki wa Syria"
5 Julai 2012Wanajeshi 75 wa Syria, wakiwemo makanali wawili na jenerali mmoja, wameasi jeshi na kujiunga na upinzani jioni ya jana. Kwa mujibu wa taarifa ya wanaharakati wa upinzani iliyotolewa leo, wanajeshi hao sasa wamekimbia nchini Uturuki. Kundi hili la wanajeshi wa jana, linafanya idadi ya wanajeshi walioasi tangu Jumatatu, sasa kufikia 350.
Upinzani wa kuung'oa utawala wa Bashar al-Assad nchini Syria, umegeuka operesheni ya kijeshi katika miezi ya hivi karibuni, ambapo waasi wamekuwa wakiyachukua na kuyaweka chini ya udhibiti maeneo makubwa ya nchi hiyo.
Kamanda wa waasi hao, Abu Alaa, ameliambia shirika la habari la Ujerumani, DPA, kwamba wanajeshi wa "serikali hawawezi kuingia kwenye maeneo kama vile Homs, Deir al-Zour na baadhi ya wilaya za Damascus," kwa kuwa yamo mikononi mwa wanamapindunzi.
China yasusa mkutano wa "Marafiki wa Syria"
Hapo kesho, Ufaransa itakuwa mwenyeji wa wawakilishi 100 kutoka mataifa ya Kiarabu na ya Magharibi pamoja na upinzani wa Syria kuujadili mgogoro huo wa miezi 16 sasa.
Mkutano huo unaofahamika kama wa "Marafiki wa Syria" unakusudia kupanga mipango ya kumalizwa kwa uwamwagaji damu.
Lakini tayari China, ambayo pamoja na Urusi ni watetezi wakubwa wa utawala wa Assad kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, imeshasema kwamba haitahudhuria mkutano huo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, Liu Weimin, amesema hivi leo kwamba kwa sasa nchi yake haifikirii kuhudhuria mkutano huo.
Mkutano huo wa Paris unafuatia ule wa mwezi Februari mjini Tunis, Tunisia, na mwengine wa mwezi Aprili wa Istanbul, Uturuki, ambayo yote ilitaka hatua kali zaidi dhidi ya utawala wa Assad.
Urusi yaituhumu Magharibi kwa upotoshaji
Marekani, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani pamoja na Saudi Arabia na Qatar ni viongozi wa kundi hilo linalojiita "Marafiki wa Syria", lenye zaidi ya wajumbe 60, yakiwemo mataifa mengi ya Umoja wa Ulaya na ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.
Urusi, mshirika wa muda mrefu wa utawala wa Assad, ilishatangulia kusema kwamba ingelijitenga kando na mkutano huo wa Paris baada ya kuyatuhumu mataifa ya Magharibi kwa kuyapotosha makubaliano ya mwishoni mwa wiki kati ya mataifa yenye nguvu huko Geneva, Uswisi, yaliyokusudia kupatikana kwa serikali ya mpito nchini Syria.
Urusi na China zilisema kwenye mazungumzo hayo, liwe ni jukumu la Wasyria wenyewe kuamua namna ya kipindi hicho cha mpito kitakavyokuwa, na kwamba Rais Assad anaweza kuwa sehemu ya serikali hiyo, lakini mataifa ya Magharibi yamekuwa yakishikilia kwamba Assad asiwemo kwenye serikali hiyo.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman