1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China na Marekani wasaka suluhu ya mzozo wa biashara

7 Januari 2019

China na Marekani wanataka kushirikiana kibiashara wakati mataifa hayo mawili yenye nguvu kubwa kiuchumi duniani yanapokutana tena kuanzisha upya mazungumzo ikiwa ni jaribio la kuhitimisha mzozo wa kibiashara baina yao. 

https://p.dw.com/p/3B8HF
China | Jeffrey D. Gerrish in Peking
Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo/A. Wong

China na Marekani wameeleza nia ya kutaka kushirikiana kibiashara, wakati mataifa hayo mawili yenye nguvu kubwa kiuchumi duniani yanapokutana tena kuanzisha upya mazungumzo ikiwa ni jaribio la kuhitimisha mzozo wa kibiashara baina yao. 

Maafisa wa Marekani wanakutana na wenzao mjini Beijing wiki hii, kwa ajili ya mazungumzo ya ana kwa ana tangu rais Donald Trump wa Marekani na rais wa China, Xi Jinping kukubali mwezi Disemba siku 90 za kusitisha mzozo wa kibiashara ambao pia umeathiri masoko ya kimataifa.

Makubaliano hayo yalifikiwa wakati viongozi hao walipokutana pembezoni mwa mkutano wa mataifa yaliyoendelea kiviwanda na yanayoinukia kiuchumi - G20 uliofanyika nchini Argentina. Kwenye mazungumzo hayo, marais hao walikubaliana kusimamisha kuwekeana ushuru mpya wa bidhaa baina yao. 

Argentinien G20 Gipfel - US-Präsident Donald Trump und Chinesischer Präsident Xi Jinping
Rais wa China, Xi Jinping na Rais Donald Trump wa Marekani, kwenye mkutano wa G20 huko Argentina.Picha: picture alliance/dpa/Maxppp

Naibu mkuu wa kitengo cha China katika baraza la biashara kati ya China na Marekani, Jacob Parker alipozungumza na shirika la habari la AP mjini Beijing amesema kuna hatua ambazo tayari zimefikiwa tangu kulipofikiwa makubaliano hayo.

"Huko nyuma, China mara kwa mara ilipokea maombi ya serikali ya Marekani na kuyakusanya pamoja lakini ilikataa kuyatekeleza kabla ya kufikiwa kwa makubaliano. Lakini kwa sasa, tumeona hatua kadhaa kupigwa na China China. Kwa mfano, tumeona ununuzi mpya wa maharage ya soya ya Marekani na ahadi ya China kuingiza mchele zaidi kutoka Marekani, jambo ambalo halikuwepo hapo awali. Tumeona pia kuchapishwa kwa rasimu ya sheria ya uwekezaji wa kigeni ambayo tumekuwa tukiisubiri tangu Januari 2015." Alisema Parker.

Rais Trump asema mazungumzo baina yao yanaendelea vizuri.

Ujumbe wa Marekani unaongozwa na mwakilishi wa Rais Donald Trump kuhusu biashara Jeffrey Gerrish.

Trump amesema hapo jana kwamba mazungumzo ya kibiashara na China yalikuwa yakiendelea vizuri na kwamba udhaifu wa uchumi wa China uliwashinikiza kufanyia kazi makubaliano yaliyofikiwa.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya China amesema nchi hizo mbili zilikubaliana kufanya mazungumzo, iliyoyaita "chanya na ya yenye tija", pamoja na mjadala wa kusuluhisha mzozo wa kiuchumi na biashara kwa kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wa mataifa hayo.

Lu alinukuliwa akisema "tangu mwanzo tulikuwa na imani kwamba mvutano wa kibiashara kati ya China Marekani si ishara njema kwa uchumi wa mataifa hayo yote ama kwa uchumi wa dunia. China ina nia njema, kwa kuzingatia misingi ya usawa na kuheshimiana ili kusuluhisha mzozo wa kibiashara wa mataifa hayo."

Rais Donald Trump mwaka jana alianzisha ushuru wa mabilioni ya dola kwa bidhaa ya China zinazoingizwa nchini mwake, hatua iliyosababisha kitisho cha shinikizo zaidi kwa China kubadilisha namna inavyoshughulikia masuala kuanzia ruzuku za viwanda hadi haki miliki na udukuzi. China pia ililipiza kisasi kwa kuziwekea ushuru bidhaa za Marekani.

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/APE

Mhariri: Gakuba, Daniel