China yaadhimisha miaka 70 ya utawala wa Kikomunisti
1 Oktoba 2019Sherehe hizo zinaadhimisha tangazo la Oktoba mosi mnamo mwaka 1949, pale kiongozi wa wakati huo Mao Zedong alipoitangaza Jamhuri ya Watu wa China kufuatia miongo miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Rais wa nchi hiyo Xi Jinping mapema Jumanne akiwa katika sherehe hizo na viongozi wengine wa chama katika uwanja waTiananmen amesema hakuna nguvu yoyote duniani inayoweza kuizuia China kusonga mbele. Amewapongeza wananchi wa China kwa kusema kwamba kwa zaidi ya miaka 70, watu wa China wa makabila tofauti wamefanya bidii kwa lengo moja la kufikia mafanikio makubwa ambayo yamepata heshima kubwa kote ulimwenguni.
"Leo, China ya kisoshalisti imesimama imara mashariki mwa ulimwengu, na hakuna nguvu inayoweza badilisha msimamo wa nchi yetu, hakuna nguvu inayoweza kuwazuia watu wa China na taifa la China kusonga mbele," amesema Xi.
Gwaride hilo lilofanyika Jumanne asubuhi limejumuisha wanajeshi ambao wamekuja kuonyesha silaha zao za teknolojia ya hali ya juu. Leo ni mara ya kwanza kwa umma kuonyeshwa makombora ya nyuklia yaliyotengenezwa makusudi kupambana na mifumo ya ulinzi ya Marekani. Maelfu ya wanajeshi wameshiriki katika gwaride hilo, huku ndege za kivita zikiwa zinapaa angani.
Gwaride hilo limefanyika kufuatia ahadi ya Xi ya kuiruhusu Hong Kong eneo lenye utawala wa pekee ndani ya Jamhuri ya Watu wa China, kushughulikia wenyewe mambo yake ya ndani ya nchi licha ya maandamano ya kuipinga serikali yaliyokiaibisha Chama cha Kikomunisti kabla ya maadhimisho ya leo ambayo ni siku muhimu kwa serikali ya China.
Maadhimisho ya leo yanaangaliwa kama moja wapo ya njia za utawala wa Chama cha Kikomunisti kuilinda sifa yake na taswira inayotaka kuionyesha ulimwengu ya kuwepo umoja wa kitaifa na ushirikiano nchini China licha ya changamoto zilizojitokeza hivi karibuni. Changamoto hizo ni pamoja na machafuko ya kisiasa Hong Kong, kupungua kwa ukuaji wa kiuchumi na vita vya kibiashara na Marekani.
Maandamano ya umma mjini Hong Kong ya takriban miezi minne yaliyojibiwa na serikali kwa kutumia nguvu yamesababisha vurugu katika koloni hilo la zamani la Uingereza. Maandamano ya Hong Kong ni changamoto ya kwanza dhidi ya Xi inayoshuhudiwa ulimengu mzima tangu aingie madarakani mnamo mwaka 2012.
dw,rtre