China yahitimisha luteka za kijeshi kuizunguka Taiwan
10 Aprili 2023Mazoezi hayo ya kijeshi yalikuwa jibu la Beijing dhidi ya hatua ya Rais Tsai Ing-wen wa Taiwan aliyekutana wiki iliyopita na Spika wa Bunge la Marekani, Kevin McCarthy, kitendo China ilishaonya kwamba kingelichochea majibu makali kutoka upande wake.
Baada ya siku tatu za mazoezi hayo yaliyoanza Jumamosi (Aprili 8), jeshi la China lilisema lilikuwa "limekamilisha kwa mafanikio majukumu ya Operesheni Upanga wa Pamoja."
Soma zaidi: Pelosi asema Marekani haitaitelekeza Taiwan
Taarifa iliyotolewa na Kamandi ya Mashariki ya Jeshi la Ukombizi wa Watu, PLA, ilisema "mazoezi hayo yalijaribu kwa kina uwezo wa pamoja wa matawi ya kijeshi kushambulia kwenye mazingira halisi."
Taarifa hiyo iliongeza kwamba wanajeshi wa China walikuwa "tayari kwa mapambano na wanaweza kupigana wakati wowote, na watakabili kwa nguvu zote "namna yoyote ya hisia za kujitenga kwa Taiwan na majaribio ya uingiliaji kati wa kigeni."
Mazoezi hayo ya kijeshi yalishuhudia Beijing ikionesha uwezo wake wa kufanya mashambulizi yanayolenga shabaha maalum ndani ya Taiwan na kukizingira kisiwa hicho, ikiwemo kukifungia kabisa kufikiwa kutoka nje.
Soma zaidi: Pelosi awasili Taipei licha ya vitisho vya China
Vyombo vya habari vya serikali ya China viliripoti kwamba ndege kadhaa za kijeshi zilifanya mazoezi ya kuifunga anga ya Taiwan.
Jeshi la China lilisema kuwa moja kati ya meli zake zinazobeba ndege za kijeshi iitwayo Shandong nayo pia ilishiriki kwenye mazoezi ya kijeshi ya siku ya Jumatatu (Aprili 10).
Taiwan yalaani, Urusi yaitetea China
Baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo ya kijeshi, wizara ya mambo ya kigeni ya Taiwan ililaani China kwa kuhujumu "amani na utulivu" kwenye kanda hiyo.
Wizara ya Ulinzi ya kisiwa hicho ilisema ilibaini kuwepo kwa meli 12 za kivita za China pamoja na ndege 91 siku ya Jumatatu.
Soma zaidi: China imerejelea vitisho vya kuishambulia Taiwan
Wizara hiyo ilisema ndege ya kivita chapa J15 iliruka kutoka meli ya Shandong na ilikuwa mojawapo kati ya ndege 54 zilizovuuka mpaka na kuingia anga ya Taiwan.
Mshirika wa karibu wa China, Urusi, ilitetea mazoezi hayo ya kijeshi, huku msemaji wa Ikulu ya Kremlin alisema "Beijing ina haki ya kulinda mamlaka yake na kujibu matendo ya uchokozi."
Marekani yatuma meli ya kijeshi
Katika hatua nyengine, Marekani, ambayo mara kwa mara imekuwa ikiitolea wito China kujizuwia kuchukuwa hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya Taiwan, ilituma siku hiyo ya Jumatatu meli yake ya kijeshi yenye uwezo wa kubeba makombora ya masafa marefu iiwayo USS Milius kwenye maeneo yanayozozaniwa katika Bahari ya China Kusini.
Soma zaidi: Je, ziara ya Blinken mjini Beijing inaweza kusaidia kurekebisha uhusiano wa Marekani na China?
Taarifa iliyotolewa na jeshi la majini la Marekani ilisema "sheria za kimataifa za usafiri kwenye bahari zinalinda haki, uhuru na matumizi salama ya bahari."
Jeshi hilo liliongeza kwamba meli yake ilipita karibu na Visiwa vya Spratly vinavyowaniwa na China, Taiwan, Ufilipino, Vietnam, Malaysia na Brunei. Visiwa hivyo viko umbali wa kilomita 1,300 kutoka Taiwan.
Kutumwa kwa meli hiyo ya jeshi la Marekani kulilaaniwa vikali na China, ambayo ilisema meli hiyo ilikuwa imeingia kwenye mamlaka yake "kinyume na sheria."
Chanzo: AFP