China yaionya Marekani kuwa inacheza na moto kuhusu Taiwan
22 Desemba 2024Serikali ya China imeionya Marekani kwa kitendo chake cha kutangaza kukiuzia silaha na kukipa msaada kisiwa cha Taiwan na kwamba kwa Marekani kufanya hivyo ni kucheza na moto.
Hapo jana rais wa Marekani Joe Biden aliidhinisha msaada wa dola milioni 571 kwa ajili ya vifaa vya kijeshi na huduma za idara ya ulinzi kwa Taiwan ikiwemo mafunzo ya kijeshi. Mbali na msaada huo, idara ya ulinzi ya Marekani ilitangaza pia mnamo siku ya Ijumaa kuwa mauzo ya vifaa vya kijeshi ya dola milioni 295 kwa Taiwan yalikuwa yamepitishwa.
Soma zaidiMacron asisisita uwepo Djibouti Ufaransa ikipoteza ngome zake Afrika.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya China imeitaka Marekani kuacha kuitumia silaha Taiwan na kuacha kile ilichokiita "hatua hatari zinazodhoofisha amani na utulivu katika mlango wa bahari wa Taiwan." Katika hatua nyingine serikali ya Taiwan imesema imeupokea kwa mikono miwili msaada huo wa Marekani ikisema unalenga kuimarisha ulinzi wake.
Taiwan ni kisiwa cha kidemokrasia chenye watu milioni 23 na serikali ya China imekuwa ikidai kuwa ni eneo lake.