1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yakabiliwa na tatizo la maji na kuenea kwa jangwa

Josephat Charo7 Juni 2006

Katika siku za hivi karibuni tatizo la mazingira lililosababishwa na kukua kwa uchumi wa China, limekuwa likijadiliwa sana. Swala kubwa ni usafi wa hewa na maji. Lakini mbali na matatizo haya yaliyosababishwa na binadamu, umma wa China unakabiliwa na changamoto kubwa ya kuenea kwa jangwa. Katika juhudi za kupambana na upepo unaobeba mchanga, viongozi wa China, wakisaidiwa na wataalamu wa Ujerumani, wanafanya mradi wa kupanda miti.

https://p.dw.com/p/CHnB
Shirika la GTZ laisaidia China kupanda miti
Shirika la GTZ laisaidia China kupanda miti

Ilani iko wazi. Polisi waliojihami na bunduki huifunga barabara pekee inayouunganisha mji wa Urumqi na mji wa Turfan. Giza hutanda mbinguni, miti hutikiswa kwa nguvu karibu ivunjike na hakuna awezaye kutoka nje ya nyumba wala gari.

Katika eneo la jangwani kazkazini magharibi mwa China mara kwa mara upepo mkali huvuma kwa kasi kubwa na kusababisha uharibifu wa misitu. Umeme na maji yanakosekana, nyumba huharibiwa.

Kwa miongo kadhaa iliyopita wakaazi wa jangwa la Taklamakan na Gobi wamejizatiti kukabiliana na hali inayowakumba. Haiba ya zamani haipo tena na ufanisi wa kiuchumi katika eneo la pwani haujafika na kuwafaidi watu wa jimbo la Xinjiang.

Mara kwa mara hutokea machafuko makali ambayo serikali ya mjini Peking huyazima kwa kutumia nguvu. Jimbo muhimu la Xinjiang, ambalo kwa mda mfupi lilimilikiwa na jamhuri ya Turkistan kati ya mwaka wa 1944 na 1945, hutumiwa na China katika vita dhidi ya ugaidi.

Sio tu machafuko ya kijamii yanayoweza siku moja kuuhatarish mji wa Peking, ulio umbali wa kilomita 2,500. Kila mara upepo mkali uliobeba mchanga mwingi husababisha wingu kubwa katika anga ya mji wa Peking.

Abiria huvaa vitambaa kuziba pua zao. Hospitalini wagonjwa wengi, hususan wazee, hutibiwa kwa matatizo ya kupumua. Ama kweli tatizo la mchanga sio tatizo pekee. Mjini Peking kuna tatizo kubwa la ukosefu wa maji kila mara.

Dr Wolfgang Schulz wa shirika la misaada ya kiufundi la Ujerumani GTZ, anasema, ´Unaweza kujionea mwenyewe baada ya usiku mmoja vumbi jingi na mchanga umekusanyika kila mahali ndani ya nyumba.

Na tatizo la pili kubwa ni ukosefu wa maji hapa mjini, kwa sababu maeneo ya kuhifadhia maji na misitu nje ya mji wa Peking, yamefunikwa na mchanga.´

Tangu mwaka wa 1978 shirika la misaada ya kiufundi la Ujerumani GTZ, limekuwa likidhamini mradi wa kupanda miti hususan katika eneo la kazkazini na kazkazini magharibi mwa Peking. Shughuli nyingi za kilimo, ukataji miti katika miongo iliyopita na maendeleo ya viwandani, yamesabisha athari zinazoweza kuonekana.

Katika kipindi kifupi kijacho kutoridhika kwa umma wa China juu ya tatizo kubwa la ukosefu wa maji na kuenea kwa jangwa kunaweza kuhatarisha mandeleo nchini humo.

Wachina wenyewe wana mradi mkubwa wa kuilinda miji yao mikubwa kwa sababu katika mji kama Peking ulio na wakaazi milioni 14, na uchumi unaoendelea kunawiri, hakuna maji tena. Ama kuna upepo mkali unaovuma na kubeba mchanga kila wakati.

Kwa hiyo ni kitu gani basi uchumi wa mji kama Peking unachoweza kuzuia? Ni mengi.

Takriban tani elfu 300 za mchanga zilianguka katika miji mikubwa ya China wakati wa tufani kali. Mradi wa kupanda miti unaojulikana kama ukuta wa kijani unaijumulisha mikoa 13 ya China.

Mradi huo umeelezwa kuwa mkubwa zaidi duniani, na miti itapandwa kwa asilimia 40 ya ardhi ya China.