1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CIA: Mohammed bin Salman aliamuru kuuawa Khashoggi

17 Novemba 2018

Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) linaamini kwamba Mwanamfalme Mohammed Bin Salman wa Saudi Arabia ndiye aliyeamrisha kuuawa kwa mwandishi wa habari Jamal Khashoggi.

https://p.dw.com/p/38QNG
Mohammed bin Salman Al Saud Kronprinz Saudi-Arabien
Picha: Reuters/A. Levy

Vyanzo kutoka ndani ya shirika hilo vililiambia shirika la habari la Ujerumani, dpa, kwamba CIA ilishaviarifu vyombo vyengine kwenye serikali ya Marekani, likiwemo baraza la Congress, juu ya ugunduzi wake huo ambao unapingana na msimamo wa serikali ya Saudi Arabia kwamba Mwanamfalme Mohammed hakuhusika na mauaji hayo.

Tathmini hiyo ya CIA, ambayo kwanza iliripotiwa na gazeti mashuhuri la Washington Post ambalo Khashoggi alikuwa akiliandikia, ni ya hali ya juu kabisa kutolewa na Marekani hadi sasa ikimuhusisha na mtawala huyo mtarajiwa wa Saudi Arabia moja kwa moja na mauaji hayo.

Maafisa wa Marekani wamekuwa na wakishuku kwamba huenda mrithi huyo wa ufalme wa Saudi Arabia alijuwa kuhusu mipango ya kumuua Khashoggi kutokana na namna anavyodhibiti masuala yote makubwa na madogo ndani ya taifa hilo tajiri kwa uzalishaji mafuta duniani, ingawa hawajawahi kutamka hadharani wasiwasi wao huo.

Ugunduzi kamili wa CIA

Gazeti la Washington Post, likiwanukuu watu walio karibu na suala hili, lilisema kuwa sehemu ya tathmini ya CIA ilitokana na mazungumzo ya simu kati ya kaka yake Mohammed bin Salman, Mwanamfalme Khaled bin Salman, ambaye ndiye balozi wa nchi yake nchini Marekani, na Khashoggi.

Jamal Khashoggi
Jamal Khashoggi aliuawa akiwa kwenye ubalozi mdogo wa nchi yake mjini Istanbul, Uturuki, tarehe 2 Oktoba.Picha: imago/IP3press/A. Morissard

Mwanamfalme Khaled alimuambia Khashoggi kuwa alipaswa kwenda kwenye ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul ili kuchukuwa nyaraka, huku akimuhakikishia kwamba ingelikuwa salama kwake kufanya hivyo.

Gazeti hilo, likiwanukuu watu walioyachunguza mazungumzo hayo ya simu, lilisema haikufahamika mara moja endapo Khaled alifahamu kuwa Khashoggi angeliuawa, lakini alipiga simu hiyo kutokana na maelekezo ya kaka yake, Mohammed bin Salman.

Gazeti la Washington Post liliandika kuwa CIA pia ilichunguza simu iliyopigwa kutoka ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul baada ya mauaji ya Khashoggi. Maher Mutreb, afisa wa usalama ambaye mara kadhaa ameonekana akiwa na Mohammed bin Salman, alimpigia simu Saud al-Qahtani, msaidizi wa ngazi za juu wa Bin Salman, akimfahamisha kuwa operesheni ilikuwa imekamilika.

Ubalozi wa Saudi Arabia wakanusha

Ikulu ya Marekani na Wizara ya Mambo ya Nje zilikataa kusema chochote juu ya suala hili, huku msemaji wa ubalozi wa Saudi Arabia mjini Washington akiita tathmini hiyo kuwa ni ya uongo. "Tumekuwa na tunaendelea kusikia dhana mbalimbali bila ya kuona jambo lolote la msingi kwenye dhana hizi," aliongezea msemaji huyo alipotakiwa maelezo yake na shirika la habari la AP.

Mwanamfalme Khaled aliandika kwenye mtandao wa Twitter siku ya Ijumaa (Novemba 17) kwamba mawasiliano yake ya mwisho na Khashoggi yalikuwa kupitia ujumbe wa maandishi ya simu ya mkononi tarehe 26 Oktoba 2017, takribani mwaka mmoja kabla ya kifo cha mwandishi huyo wa habari.

"Sikuwahi kuzungumza naye kwa simu na kamwe sikuwahi kumtaka aende Uturuki kwa sababu yoyote ile. Ninaitaka serikali ya Marekani kutoa taarifa yoyote kuhusiana na madai haya," aliandika Khaled.

Khashoggi alikataa kurejea Saudi Arabia

Türkei, Istanbul: Yasin Aktay spricht auf der symbolischen Beerdigung Kashoggis
Sala ya Maiti kwa ajili ya Jamal Khashoggi iliyofanyika mjini Istanbul siku ya Ijumaa tarehe 16 Novemba 2018.Picha: Reuters/M. Sezer

Khashoggi, mkosoaji mkubwa wa serikali ya Saudi Arabia, aliuawa kwenye ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul tarehe 2 Oktoba, wakati alipokwenda kuchukuwa nyaraka alizohitaji kwa ajili ya kufunga ndoa na mwanamke wa Kituruki.

Khashoggi alikuwa amekataa shinikizo la kumtaka arejee nchini Saudi Arabia. Maafisa wa Saudia walisema kikosi cha watu 15 kilitumwa kumkabili kwenye ubalozi huo mdogo na alikufa kwa bahati mbaya akiwa ametiwa kabari na watu waliotumwa kumrejesha Saudi Arabia.

Tangu awali maafisa wa Uturuki wamekuwa wakisisitiza kuwa mauaji hayo yalikuwa ya makusudi na wamekuwa wakiishinikiza Saudi Arabia kuikabidhi Uturuki waliohusika na mauaji hayo kwa ajili ya kushitakiwa. Mshauri mmoja wa Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki aliishutumu Saudi Arabia kwa kujaribu kuyafichaficha mauaji hayo. 

Mwendesha mashitaka wa Saudi Arabia, Shalaan al-Shalaan, alisema siku ya Alhamis (16 Novemba) kwamba anaiomba mahakama kutoa hukumu ya kifo kwa watuhumiwa watano walioshitakiwa kwa mauaji hayo. 

Hata hivyo, mwendesha mashitaka huyo aliwaambia waandishi wa habari kwamba Mwanamfalme Bin Salman hakuwa akijuwa chochote kuhusu operesheni hiyo ambayo ilishuhudia mwili wa Khashoggi ukikatwakatwa vipande vipande na kuondolewa kwenye ubalozi. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/dpa/Reuters
Mhariri: Yusra Buwayhid