Clinton aendelea na ziara yake Afrika Kusini
7 Agosti 2012Katika hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano huo, Clinton alisema Marekani inataka kuimarisha biashara na Afrika, huku uchumi wa eneo hilo ukikua licha ya mzozo wa kiuchumi unaoikabili dunia. Alisisitiza umuhimu wa kutanua biashara pamoja na mahusiano ya kidiplomasia na Afrika kusini. Alisema ingawa tayari amezitembelea nchi sita za Afrika, amekuwa akitoa ujumbe mmoja: "Tunataka ushirikiano wa muda mrefu barani Afrika utakaoongeza manufaa kwa Waafrika badala ya kuyapunguza.
Hata hivyo viongozi wa kibiashara kwenye mkutano huo walikiri kwamba kuna changamoto za kufanya biashara barani Afrika, ikiwa ni pamoja na kuyumba kwa hali ya kisiasa na hofu ya kutaifishwa kampuni binafsi na serikali. Huku viongozi wa Afrika kusini wakiahidi kufungua soko la nchi hiyo kwa ajili ya biashara, baadhi ya wanasiasa nchini humo wanaendelea kuzungumzia uwezekano wa kuzitaifisha kampuni za madini na kampuni nyingine.
Akiuhutubia mkutano wa Johannesburg hapo jana, naibu waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Marekani anayeshughulikia masuala ya ukuaji wa kiuchumi, Robert Hormats, alisema kampuni za Marekani zinatafuta nchi nyingine kufanya nazo biashara.
"Kuna nafasi kubwa kwa kampuni za Marekani kushirikiana na kampuni za Afrika Kusini na tunaona uwezekano wa kampuni zaidi kufanya hivyo. Tunafikiri kampuni za Marekani zinaweza kuongeza manufaa kupitia mafunzo, ubora wa bidhaa zinazotengeneza na ubora wa uwekezaji zinazofanya."
Mkataba wa mkopo kusainiwa
Maafisa wa Marekani na Afrika kusini wanatarajiwa leo kusaini mkataba rasmi wa mkopo wa Marekani kwa Afrika kusini utakaosaidia miradi ya nishati inayoweza kutumika tena na tena. Marekani itaipa Afrika kusini mkopo wa hadi dola bilioni 82 kugharamia miradi hiyo itakayozihusisha kampuni za Marekani. Mkopo huo wa miaka 18 utatolewa na benki ya Marekani ya uuzaji na uagizaji bidhaa katika nchi za nje. Rais na Mwenyekiti wa benki hiyo, Fred Hochberg, amesema fedha hizo huenda zikatumiwa kwa miradi ya nishati inayotokana na upepo, jua na chemichemi za maji.
Waziri Clinton ameandamana na ujumbe mkubwa katika ziara yake wakiwemo viongozi wa wakala za serikali zikiwemo za uchumi, biashara na maendeleo pamoja wajumbe wa kampuni binafsi kama vile Chevron na Wal-Mart. Atakutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Afrika kusini, Maite Nkaone-Mashabane na viongozi wengine wa serikali na biashara.
Clinton aliwasili jana Afrika kusini akitokea nchini Malawi na kukutana na rais wa zamani wa nchi hiyo, Nelson Mandela, katika kiji chake cha Qunu, katika jimbo la Cape Mashariki. Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marakeni atakamilisha ziara yake Afrika kusini Alhamisi wiki hii, na ataendelea na ziara yake ya Afrika kwa kuzitembelea Nigeria na Benin.
Mwandishi: Josephat Charo/Subry Govender/APE
Mhariri: Daniel Gakuba