Clinton aitembelea Afghanistan
7 Julai 2012Waziri huyo wa Marekani amewasili Afghanistan akitokea Paris, Ufaransa, ambako alikuwa akihudhuria mkutano wa marafiki wa Syria ulioshirikisha nchi 100.
Clinton atakutana na Rais Hamid Karzai kwa ajili ya mazungumzo kuhusu mahusiano ya kiraia na kijeshi baina ya nchi zao. Watazungumza pia kuhusu juhudi zilizokwama za mapatano nchini humo.
Baada ya mazungumzo hayo, Clinton ataelekea Japan kuhudhuria mkutano wa kimataifa wenye lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya nchi hiyo kupatiwa misaada utakaofanyika Jumapili (8 Julai). Wafadhili wanatarajiwa kuchangia kiasi cha dola bilioni nne za Marekani zitakazotumika kwa mahitaji mbalimbali ya wananchi wa taifa hilo katika kipindi cha mwaka mmoja.
Akataa kuweka wazi msaada wa Marekani kwa Afghanistan
Hata hivyo yeye na maafisa wengine wa Marekani alioambatana nao, wamekataa kutaja kiwango ambacho nchi hiyo itachangia kwenye mkutano huo mjini Tokyo na pia kiasi gani kinatarajiwa kukusanywa jumla. Jumuiya ya kimataifa iko kwenye harakati za kuisaidia nchi hiyo kuinua uchumi wake na kuilinda isurudi kwenye matatizo ya awali baada ya kuondoka kwa vikosi vya kigeni ifikapo mwishoni mwa mwaka 2014.
Benki Kuu nchini humo imesema kuwa kiasi kinachohitajika ni dola za Marekani bilioni sita kwa mwaka ili kuongeza kasi ya ukuaji uchumi kwa kipindi cha muongo mmoja ujao.
Hata hivyo Afisa mmoja aliyeambatana na Clinton amesema kuwa mchango wa Mrekani na ule wa jumuiya ya kimataifa utakuwa chini ya kiwango.
Kiwango kikubwa cha ukusanyaji wa fedha hizo za msaada kilikuwa mwaka 2010 ambapo dola bilioni za Marekani zilipatikakana huku theluthi mbili ya kiasi hicho ikitolewa na Marekani. Sasa wafadhili na mataifa yanayolinda amani nchini humo yanajiuliza ni kwa muda gani jumuiya ya kimataifa itakuwa radhi kuisaidia Afghanistan.
Hofu ya kushuka kiwango cha misaada
Maafisa wa Marekani wanasema kuwa wanatarajia nchi zinazoshiriki mkutano huo zitaahidi kuendelea kuisaidia Afghanistan kwa kiwango kilekile au angalu kinachokaribiana na cha miaka ya hivi karibuni lakini wamekiri pia kuwa moyo wa kufanya hivyo unazidi kufifia.
Baadhi ya wafadhili wakuu na mashirika ya misaada yameonya kuwa kushuka kwa nia ya kutaka kuisaidia nchi hiyo kunaweza kusababisha fedha na misaada isiwafikie raia kwa wakati na hivyo mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya na elimu kupotea.
Wakiondoa hofu kuhusu masuala hayo, Maafisa hao wamesema kuwa kiwango kitakachopatikana kitatosha kuonyesha kuwa jumuiya ya kimataifa inatimiza ahadi yake kwa Afghanistan.
Marekani inasita kutaja kiwango cha pesa zitakazotolewa kwa Afghanistan kutokana na ukweli kuwa jumla ya pesa hiyo inatoka kwa nchi hiyo.
Mwandishi: Stumai george/AFP/APE
Mhariri: Sekione Kitojo