1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton asomba kura South Carolina

28 Februari 2016

Mgombea Urais wa Marekani Hilary Clinton amepata ushindi mkubwa dhidi ya Bernie Sanders katika uchaguzi wa mchujo wa chama cha Democratic katika jimbo la South Carolina kuwania uteuzi wa mgombea urais wa chama hicho

https://p.dw.com/p/1I3lK
Mgombea urais wa Marekani wa chama cha Demokratik Hilary Clinton akiwapungia wafuasi wake South Carolina.(27.02.2016)
Mgombea urais wa Marekani wa chama cha Demokratik Hilary Clinton akiwapungia wafuasi wake South Carolina(27.02.2016)Picha: Reuters/J. Ernst

Mgombea Urais wa Marekani Hilary Clinton amepata ushindi mkubwa dhidi ya Bernie Sanders katika uchaguzi wa mchujo wa chama cha Democratic katika jimbo la Carolina Kusini kuwania uteuzi wa mgombea urais wa chama hicho.

Ushindi huo wa Jumamosi (27.02.2016) unampa Clinton msukumo kabla ya siku muhimu kabisa ya uchaguzi huo wa mchujo : yaani mpambano wa "Jumanne Kabambe" ambapo majimbo 11 yatapiga kura kuchaguwa wagombea wa kupeperusha bendera za vyama katika uchaguzi wa rais wa Marekani baadae mwaka huu.

Baada ya wiki nne za uchaguzi wa mchujo kuwania kuingia Ikulu ya Marekani Clinton waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje amejipatia ushindi wake wa kwanza muhimu katika kampeni yake baada ya ule wa kibaruwa kigumu wa Iowa na kushindwa na Sanders huko Hampshire na halafu ushindi wa pointi nne wa Nevada.

South Carolina ni jimbo la kwanza la kusini kupiga kura kuteuwa mgombea wa kukiwakilisha chama cha Demokratik katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2016 kabla ya uchaguzi huo wa mchujo kuingia katika majimbo mengine 11 nchini kote.

Marekani haikuacha kuwa adhimu

Clinton amesema huku akishangiliwa na umati kwamba "Kesho kampeni hii inaingia ngazi ya taifa " akiwashukuru wafuasi wake huko Columbia South Carolina ambapo ameibuka na ushindi unaomfungulia njia ya kuteuliwa kuwa mgombea wa urais wa chama hicho amesema " Tataigombania kila kura katika kila jimbo.Hatukichukulii kitu chochote, wala mtu yeyote kwa mzaha".

Wafuasi wa gombea urais wa Marekani wa chama cha Demokratik Hilary Clinton wakisheherekea ushindi wake wake South Carolina .(27.02.2016)
Wafuasi wa gombea urais wa Marekani wa chama cha Demokratik Hilary Clinton wakisheherekea ushindi wake wake South Carolina .(27.02.2016)Picha: Reuters/R. Hill

Clinton pia alimdhihaki mtu ambaye wengi wanamuona kuwa yumkini akawa mgombea wa urais wa chama cha Republican : Donald Trump ambaye kauli mbiu ya kampeni yake ni "Ifanye Amerika Adhimu".

Clinton amesema "Licha ya kile mnachokisikia, hatuna haja ya kuifanya Marekani iwe adhimu tena. Marekani katu haikuwahi kuacha kuwa adhimu."

Ameongeza kile wanachotakiwa wafanye ni "kuifanya tena Marekani iwe kitu moja " ikiwa ni hoja dhidi ya kauli za majigambo zinozopendelewa na Trump zenye kugawa watu ambazo zinachochea chuki dhidi ya wahamiaji, Waislamu na wapinzani wake.

Ushindi wamkombowa Clinton

Wakati asimia 99 ya maeneo yaliyopiga kura matokeo yake yakiwa yamepatikana Clinton alijizolea asilimia 73.5 dhidi ya asilimia 26 alizopata Sanders.

Hillary Clinton katika harakati za kampeni nchini Marekani.
Hillary Clinton katika harakati za kampeni nchini Marekani.Picha: Reuters/D. Becker

Ushindi huo kabambe umemkombowa Clinton ambaye mwaka 2008 alishindwa vibaya katika jimbo hilo na Barack Obama ambaye ushindi wake hapo ulikuwa nukta muhimu kwa kampeni yake ya mafanikio na kuja kuchaguliwa kuwa rais.

Kura za awali katika jimbo hilo la South Carolina zinaonyesha Wamarekani wenye asili ya Kiafrika ambao wanawakilisha asilimia 61 wa chama cha Demokratic katika uchaguzi huo wa mchujo walimuunga mkono Clinton kwa asilimia 86 kuliko vile walivyomuunga mkono Obama miaka minane iliopita.

Kwa uangalifu Clinton amewashawishi wapiga kura weusi kwa kiasi fulani kwa kumpongeza Obama na kwa kuahidi kuendeleza haiba yake.

Pia amekuwa akiendesha kampeni yake hiyo bega kwa bega na maskofu weusi na kuzuru makanisa ya Wamarekani wenye asili ya Kiafrika na vyuo vya weusi vya kihistoria.

Ari ya Sangers bado iko juu

Sanders ambaye anajieleza kuwa yeye ni mjamaa wa chama cha Democratic anayetaka kuanzisha mapinduzi ya kisiasa nchini Marekani tayari anaangalia mbele baada ya kushindwa South Carolina.

Bernie Sanders anawania ateuliwe awe mgombea wa urais wa chama cha Demokratik nchini Marekani.
Bernie Sanders anawania ateuliwe awe mgombea wa urais wa chama cha Demokratik nchini Marekani.Picha: Reuters/J. Young

Mapema Jumamosi ameelekea Texas na baadae Minnesota majimbo mawili ambayo yatapiga kura hapo Jumanne wakati seneta huyo wa Vermont anapohitaji kuendelea kuonyesha ari yake iwapo anataka kuzidi kumpa changamoto Clinton katika uchaguzi huo wa mchujo.

Sanders alimpongeza Clinton lakini amesisitiza kwamba yuko tayari kwa mpambano wa muda mrefu wa kampeni. Amesema katika taarifa baada ya kutolewa kwa matokeo kwamba "Nataka ifahamike wazi kwa kitu kimoja usiku huu.Kampeni hii ndio kwanza imeanza."

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Gakuba Daniel