1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton na Trump kuchuana kwa mdahalo wa mwisho

Caro Robi
19 Oktoba 2016

Mgombea urais wa chama cha Democratic Hillary Clinton na wa Republican Donald Trump leo wanakutana katika mdahalo wa mwisho wa wagombea urais nchini Marekani kabla ya uchaguzi utakaofanyaika tarehe 8 Novemba.

https://p.dw.com/p/2RR8U
US TV Debatte Trump vs Clinton
Picha: picture alliance/AP Photo/J. Locher

Huku zikisalia chini ya wiki tatu kabla ya uchaguzi mkuu nchini Marekani, kura za maoni zinaonyesha Bi Hillary Clinton anaongoza dhidi ya mpinzani wake Donald Trump. Mdahalo utakaofanyika leo usiku katika chuo kikuu cha Las Vegas katika jimbo la Nevada utampa Trump kile kinachoonekana fursa yake ya mwisho kubadilisha mkondo wa kampeini zake ambazo zimekumbwa na misururu ya kashfa zikiwemo kuwadhalilisha kingono wanawake.

Clinton amekuwa hajionyeshi sana katika siku za hivi karibuni akijifungia na washirika wake katika hoteli moja karibu na nyumbani kwake mjini New York kujiandaa kwa mdahalo huo utakaoonyeshwa kwa dakika 90 kupitia televisheni.

Wagombea wote wawili wameshafika katika jimbo la Nevada tayari kuchuana katika mdahalo huo wa mwisho kabla ya uchaguzi wa urasi tarehe 8 mwezi ujao. Utaendeshwa na mwanahabari wa kituo cha televisheni cha Fox Chris Wallace na mamilioni ya watu wanatarajiwa kuufuatilia.

Katika duru hii ya mdahalo, wagombea hao wataulizwa kuhusu madeni ya kitaifa, suala la uhamiaji, uchumi, mahakama ya juu, sera za kigeni na uwezo wao wa kuwa raia. Katika midahalo miwili iliyopita, Trump na Clinton walipapurana vikali kwa kurushiana maneno makali na shutuma nyingi kiasi cha kughubika mada zilizopaswa kujadiliwa.

USA Presidentschaftsdebatte - Donald Trump und Hilary Clinton
Wagombea urais Marekani Hillary Clinton na Donald TrumpPicha: Getty Images/AFP/T. A. Clary

Wachambuzi wanasema Clinton anapaswa kuendelea kuwa mtulivu na kujiamini huku Trump akitarajiwa kujifunza kutoka kwa midahalo iliyopita na kunoa makali dhidi ya Bi Clinton kuhusu Syria na Libya.

Kura za maoni za zinaonyesha Bi Clinton akiongoza kwa umaarufu kwa asilimia 46, Trump akiwa na asilimia 39 na mgombea wa tatu Gary Jonhnson akiwa na asilimia 6.4. Trump amevishutumu vyombo vya habari kwa kuegemea upande wa mpinzani wake na hata kuutilia shaka mfumo wa uchaguzi Marekani akilalamika kuna njama ya udanganyifu wa kura.

 

Licha ya kuwa Clinton anakubalika zaidi na umma, tangu mwanzo wa kampeini zake, anakumbwa na mashaka kama ni mkweli au kiongozi wa kuaminika hasa kutokana na kashfa za barua pepe alipokuwa waziri wa mambo ya nje. Tayari chaguzi za mapema zinaendelea katika baadhi ya majimbo Marekani.

Malik Obama nduguye Rais wa Marekani anayemuunga mkono Trump amealikwa na Trump kuhudhuria mdahalo wa leo usiku na Clinton amemualika bilionea wa Marekani Mark Cuban ambaye ni mkosaji mkubwa wa Trump kuhudhuria.

Mwandishi: Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Gakuba Daniel