Clinton ziarani Afrika Kusini
6 Agosti 2012Ziara ya Hillary Clinton nchini Afrika Kusini imeanzia kwa chakula cha mchana na Mandela ikiwa ni hatua ya kuonesha jinsi anavyoendelea kupewa heshima kiongozi huyo wa zamani aliyeongoza mapambano dhidi ya utawala wa Wazungu walio wachache.
Mzee Madiba, kama ulivyo umaarufu wa Mandela, ambaye hali yake ya afya yake imekuwa mbaya kutokana na umri ni mtu ambaye sio tu anawawakilisha mashujaa wa dunia bali pia ni mtu ambaye Clinton anamuangalia kama rafiki wake wa karibu. Kama alivyosema afisa mmoja wa Marekani ni Clinton amejifunza mengi mno kutoka kwa Mzee Madiba.
Mandela alichaguliwa kuwa rais wa Afrika Kusini baada ya kufanyika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia uliowahusisha watu wa rangi na matabaka yote nchini humo mwaka 1994 ikiwa ni baada ya kukaa jela kwa miaka 27 kama mfungwa wa kisiasa chini ya utawala wa ubaguzi wa rangi ''Apatheid''. Wakati huo mumewe Hillary Clinton, Bill Clinton ndiye aliyekuwa rais wa Marekani, tangu wakati huo familia hizo mbili zikaanza urafiki wa karibu.
Bill Clinton alifanya ziara nyumbani kwa Mandela, Qunu, mwezi uliopita katika mkesha wa sherehe za siku ya kuzaliwa kwake miaka 94 iliyopita.Hillary Clinton alikutana na Mandela kiasi miaka mitatu iliyopita nyumbani kwake Johannesberg ambapo alimpongeza kutokana na ushawishi aliokuwa nao katika maisha yake.
Katika ziara yake hii Clinton amesema Mandela amefanya mengi ya mafanikio sio tu kwa ajili yake binafsi lakini kwa Waafrika Kusini na Ulimwengu kwa ujumla.Masuala anayopanga kuzungumza na viongozi wa kisiasa akiwa katika ziara hiyo ni pamoja na ushirikiano wa kibiashara kati ya Marekani na Afrika Kusini.
Ziara hiyo itakamilika alhamisi ambapo waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani ataelekea Nigeria na Benin.Aidha anatazamiwa kufika Ghana kuhudhuria maziko ya kitaifa ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo John Atta Mills kabla ya kwenda Uturuki kwa ajili ya mazungumzo juu ya mgogoro wa Syria.
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed Khelef